Home BIASHARAUWEKEZAJI Marekani yapongeza juhudi za Tanzania katika kuvutia wawekezaji

Marekani yapongeza juhudi za Tanzania katika kuvutia wawekezaji

0 comment 104 views

Na Grace Semfuko –MAELEZO

Serikali ya Marekani imesema inatambua juhudi za Serikali ya Tanzania za kuvutia wawekezaji na kwamba Mazingira mazuri ya uwekezaji yanayofanywa na Serikali yatasaidia kufikia Uchumi wa kati na wa Viwanda.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt Inmi Patterson amesema kufuatia juhudi hizo Serikali yake inaungana na Tanzania katika kuwezesha wawekezaji wengi wa Kimarekani kuja kuwekeza nchini.

Balozi Patterson ameyasema hayo Jijini Dar es salaam, alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Geoffrey Mwambe alipomtembelea Ofisini kwake na kuzungumzia masuala mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo  namna bora ya kuvutia wawekezaji wa nje.

Kaimu Balozi huyo ameihakikishia Serikali ya Tanzania kwamba itatoa kila aina ya ushirikiano ili kufanikisha Tanzania ya viwanda.

“Ubalozi wa Marekani,nchi ya Marekani na Wamarekani wote waliopo nchini Tanzania wapo tayari kusaidiana na serikali katika kuhakikisha nchi ya viwanda inafanikiwa,” amesema.

Pia ametoa ushauri kwa Serikali ya Tanzania kuwa ili ifanikiwe kwenye uchumi wa viwanda ni vema ikaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kufanikisha uwekezaji na kwamba amefurahishwa na mazungumzo ambayo Serikali ya Tanzania inafanya kati yake na sekta binafsi.

“Hakuna nchi ambayo inaweza kufikia uchumi wa viwanda bila kushirikisha sekta binafsi  pamoja na wawekezaji wa ndani na nje. Hivyo ni vema sekta binafsi zikapewa fursa katika uwekezaji ili kufikia Serikali ya Viwanda ambayo sisi tunaiunga mkono kwa nguvu zote,” amesema.

Kuhusu mazungumzo yao amesema yamejikita katika kukuza biashara ,uwekezaji na kukuza uchumi na kwamba kutokana na mazingira mazuri yaliyopo ni imani yao Tanzania itafikia kuwa nchi ya viwanda.

Kwa upande wake Mwambe amesema TIC jukumu lao ni kukutanisha sekta mbalimbali za Serikali na binafsi ambapo mabalozi wa Tanzania waliopo nchi mbalimbali wanahakikisha wanashiriki kikamilifu kuvutia kuvutia wawekezaji.

Amefafanua ni hivyo hivyo kwa ubalozi wa Marekani nchini kupitia Kaimu Balozi wake wamekuwa na wajibu wa kuhamasisha uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

“Ni jukumu lake kuhamasisha wawekezaji wa Marekani kuja Tanzania kuwekeza.Tunafahamu juhudi za Serikali ya Marekani katika kuisaidia Tanzania kwa kuhakikisha inajiimarisha kiuchumi.

Amesema jitihada za Kaimu Balozi zimesaidia kufanikisha kwa ujio wa kundi la wafanyabiashara wa Florida kuja nchini kwa ajili ya kuangalia mazingira ya uwekezaji na kwamba wanatarajia kuja siku za karibuni.

” Tumezungumza maeneo mbalimbali ambayo tunaweza kushirikiana ili kutimiza malengo ya Serikali ya kutekeleza uwekezaji nchini. Kama nchi tunataka kuendelea,lazima tutafute njia sahihi za kuendeleza mifumo ya uwekezaji.

“Tunataka kujenga nchi,hivyo tuna jukumu kubwa la kujenga sekta binafsi na tukiwa na private sekta tutakwenda vizuri kama Taifa.Sisi TIC tutahakikisha sekta binafsi inaimarika na maamuzi ya Serikali ni kuijenga sekta binafsi na mjumbe wa bodi yangu ni mtu mmoja kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Bw.Godfrey Simbeye,” amefafanua.

Ameongeza Serikali yenye rushwa huwa haikusanyi kodi huo ni msemo wa Mwalimu Nyerere, hivyo jukumu lililopo ni  kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatunufaisha wote.”TIC tunataka kutengeneza umoja na mazingira yanayokubalika kwenye uwekezaji zaidi”.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter