Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa pongezi kwa mabalozi ambao wamekuwa wakitafuta fursa mbalimbali hasa za kiuchumi kama ambavyo waliagizwa na Rais John Magufuli. Mwijage amesema kuwa jitihada za mabalozi hao zimepelekea wafanyabiashara kutoka nje kufika nchini kwa lengo la kuwekeza.
Waziri huyo amesema hayo jijini Dar es salaam alipokutana na waandishi wa habari. Amefafanua kuwa kazi hiyo ilikuwa inafanywa na mawaziri husika hapo awali lakini kutokana na mawaziri kutosafiri tena, mabalozi wamebeba jukumu hilo na wamekuwa wakifanya kazi kubwa kutekeleza agizo hilo.
Hadi sasa, wafanyabiashara kutoka China, Ufaransa na Ujerumani wameshawasili nchini na wamepata nafasi ya kuelezwa fursa zilizopo pamoja na taratibu na sheria za kufuatwa ikitokea muwekezaji kutoka nje atahitaji kuwekeza.