Katika kuendelea kukuza biashara na kutangaza biashara kimataifa, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mwongozo wa fursa za biashara na uwekezaji wakati wa Mkutano na Wanachama wa Chemba ya Biashara ya Marekani.
Mkutano huo, umefanyika Washington DC nchini Marekani.
Mwongozo huo uliandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara ya Marekani (U.S Chamber of Commerce) ukilenga kuainisha fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania ili kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa M. Khamis ameeleza kuwa mwongozo huo umeangazia sekta zote za uchumi pamoja na mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuhamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuchagua Tanzania kama sehemu sahihi kwa biashara na uwekezaji.
Mwongozo huo utasambazwa kwa wanachama zaidi ya milioni tatu wa Chemba ya Biashara ya Marekani.