Na Mwandishi wetu
Katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imekabidhi nyaraka za ardhi yenye ukubwa wa hekta 774 kwa uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kwa ajili ya kuendesha kilimo cha miwa. Dk.Shein alitoa agizo hilo hivi karibuni akitaka kiwanda hicho kipewe ardhi ya ziada ili kuzalisha miwa ambayo itatumika kutengeneza sukari.
Baada ya kukabidhi hati za ardhi kwa kiwanda hicho, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohamed amepongeza kiwanda hicho kwa kujipanga vema katika masuala ya uwekezaji akisema kuwa kuna eneo dogo sana la ardhi ya kilimo Zanzibar hivyo kuna haja ya viongozi kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia za kisasa zitakazowezesha uzalishaji wa mazao mengi katika eneo dogo.
Kwa upande wake, Meneja biashara wa kiwanda hicho Pranav Shah mbali na kufarijika na jitihada za haraka zilizofanywa na serikali kuwapatia eneo hilo, amesema kuanzia sasa malighafi ya miwa itapatikana kwa urahisi kwani imekuwa changamoto kubwa katika uzalishaji wa sukari hapo kiwandani kutokana na uhaba wa eneo.