Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania, Italy watia saini mkataba wa 1bn

Tanzania, Italy watia saini mkataba wa 1bn

0 comment 144 views

Tanzania na Italia, kupitia Shirika lake la Maendeleo (AICS), zimetia saini mkataba wa msaada wa Euro 410,000 (sawa na shilingi Bilioni 1).

Msaada huo ni kwa ajili ya programu ya kuimarisha mfumo wa takwimu na usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano mkoani Tanga.

Mkataba huo umetiwa saini katika Ofisi za Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipangona Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Italia nchini, Marco Lombardi, kwa niaba ya Serikali ya Italia.

Akiongea baada ya kusaini mkataba huo, Dkt. Natu Mwamba, amesema msaada huo utawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kusajili watoto 348,391 wenye umri chini ya miaka mitano katika kata 245, zilizoko katika wilaya 11 za mkoa wa Tanga kupitia vituo 650 vitakavyotumika kusajili watoto hao.

Dkt. Mwamba ameishukuru Italia kwa ushirikiano mkubwa wa kimaendeleo ambapo hivi karibuni nchi hizo mbili zimesaini mkataba wa mkopo nafuu wa Euro milioni 19.7 ambao umechanganywa na msaada wa Euro laki 2 kwa ajili ya kuboresha vyuo vya elimu ya juu vya ufundi.

Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia-Karume, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Taasisi ya Teknolojia – Dar es Salaam.

Kwa upande wake Balozi Lombardi, amesema serikali ya Italia AICS, inathamini uhusiano wake na Tanzania na inadhamiria kuwekeza zaidi kwenye uchumi wa buluu, sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji, kuwezesha wanawake kwa kuwa maendeleo ya Tanzania ndiyo maendeleo ya Italia.

“Serikali ya Tanzania inaonesha mwamko katika kusimamia uchumi kupitia Rais wake Dkt. Samia Suluhu Hassan, na sisi Italia tutazidi kuunga mkono juhudi hizi ili kufanikisha maendeleo ya nchi hii na uhusiano wa nchi hizi” ameeleza balozi Lombardi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter