Kipengele cha uwekezaji kimechukua nafasi kubwa katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2019/2020 bungeni Dodoma, ambapo wabunge mbalimbali wameitaka serikali kukipatia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mamlaka ya uamuzi ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji nchini. Mbunge wa Mufindi Mjini (CCM) Cosato Chumi, amesema kutokana na kituo hicho kutokuwa na mamlaka ya uamuzi, shughuli nyingi za uwekezaji zinacheleweshwa.
“Kule Mufindi kuna kampuni inaajiri watu 1,000 kuvuna gundi na wanataka kutengeneza kiwanda kwa ajili ya kuchakata (gundi), lakini sasa hivi ni miezi minane hawajapata hati kutoka National Land Allocation Committee (kamati ya ugawaji wa Ardhi ya Taifa)”. Amesema Chumi.
Naye Mbunge wa Wawi (CUF), Ahmed Juma Ngwali amechangia haya kuhusu mjadala wa TIC kutokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi.
“TIC ilianzishwa kwa ajili ya kuisaidia nchi katika uwekezaji lakini cha kusikitisha wawekezaji wanapata tabu sana, utakuta mkuu wa mkoa, wilaya, Osha (Wakala wa usalama na Afya Mahali pa kazi ), ofisa wa TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa) wote wana mamlaka ya kumkamata mwekezaji. Tena wanaita wanahabari na kumuonyesha hadharani, mtu ambaye ameajiri watanzania, Serikali mtuambie mnaona fahari gani kwa jambo hili? Mtu anaonyeshwa kama jambazi, hawa wawekezaji wanaambiana”. Ameeleza Ngwali.
Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni amesema kuna mambo ambayo yanakinzana katika sekta ya uwekezaji, jambo ambalo linafanya wawekezaji wakimbie. Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Grace Tendega amesema mazingira mabovu na magumu ndio yanayokwamisha sekta hiyo na kuitaka serikali kupunguza mlolongo wa kodi na kuboresha mazingira kwa wawekezaji.