Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, amewahakikishia wafanyabiashara na makampuni binafsi kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuwawezesha kuendelea kuwekeza na kukuza uchumi wa nchi.
Mafuru ametoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) Takashi Araki.
Amesema Sekta Binafsi ina imani na Serikali hali ambayo inawawezesha wawekezaji kuwa na uhakika na mipango yao.
“Kampuni ya Sigara nchini wamefurahishwa na Sera za usimamizi wa uchumi ambazo zimeendelea kuboreka na kuwawezesha kufanyabiashara yenye tija”, ameeleza Mafuru.
Amesema kampuni hiyo imeelezea kufurahishwa kwao na mazingira ya siasa yalivyo, ambayo yanaruhusu amani na utulivu huku wakiiomba Serikali kuangalia vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha ufanyajibiashara nchini kwa ufanisi zaidi.
Aidha,amesema wameshauri Serikali iangalie suala la kodi kwa kuwa na kodi ambazo zinatabirika na zisizobadilika badilika kila wakati pamoja na kuangalia mazingira mengine ya ufanyaji biashara.
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Takashi Araki amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi wa nchini huku akisisitiza kuhusu kujenga uaminifu kati ya Serikali, Sekta Binafsi na wananchi.
Amesema ni jambo la msingi kuwa na uchumi unaokua na kuhusisha maendeleo ya watu, hivyo anatamani Tanzania iwe na uchumi thabiti.