Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ametoa agizo kwa wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za Hanang, Mbulu, Kiteto, Babati na Simanjiro mkoani humo kuandaa mazingira salama kwa ajili ya shughuli za uwekezaji na kuweka mikakati ambayo itawashawishi wawekezaji kufika maeneo yao na kuwekeza.
Mnyeti ametoa agizo hilo alipokuwa katika kikao cha wadau wa maendeleo mkoani humo ambapo pia alipokea taarifa ya tafiti ya fursa za uwekezaji kutoka TIRDO.
Ameongeza kuwa, hali ya viongozi kusubiri wawekezaji waje wenyewe imechangia kwa kiasi kikubwa mkoa huo kuwa nyuma kimaendeleo kwani wawekezaji wanahitaji ushawishi na mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji.
Mbali na hayo, Mkuu huyo amesema serikali ya Manyara ipo tayari kushirikiana na wawekezaji watakaofuata taratibu na sheria kwa kusikiliza maoni yao kuhusu utoaji wa leseni na hati kupitia wakurugenzi watendaji wa halmashauri ili kuondoa urasimu usio wa lazima.