Home BIASHARA Vikwazo nane vyaondolewa Tanzania, Zambia, vyabaki 16

Vikwazo nane vyaondolewa Tanzania, Zambia, vyabaki 16

0 comment 225 views

Tanzania na Zambia zimekubaliana kuendelea kuondoa vikwazo mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi ambapo mpaka sasa vikwazo nane vimeondolewa kati ya 24 vilivyoainishwa na serikali hizo mbili.

Makubaliano hayo ni pamoja na kuondoa urasimu, kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara, kuitumia vyema miundombinu inayounganisha nchi hizo na kuruhusu muingiliano wa watu.

Hayo yamejadiliwa mjini Lusaka wakati wa kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia na kwa pamoja wakakubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo, kwenye ziara ya siku tatu ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia.

“Nafarijika kuwaambia Watanzania na ndugu zetu wa Zambia kuwa kati ya vikwazo 24 ambavyo tuliviainisha tayari vikwazo nane tumeshaviondoa kabisa na vikwazo vilivyobaki 16, hivi tumekubaliana hadi inapofika tarehe 31,12 2023 tuwe tumemaliza vikwazo vyote vile vya zamani tulivyokuwa navyo 24” ameeleza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji.

Amebainisha kuwa serikali hizo mbili zitaendelea kushughulikia vikwazo vinavyoendelea kuibuka hatua kwa hatua.

“Mimi pamoja na Waziri mwenzangu wa Biashara hapa Zambia ndugu yangu Chipoka Mulenga tumekubaliana kuwa tunafanya vikao kila wiki kupitia mtandao na kila baada ya mwezi tuwe na kikao cha site, kikao ambacho ni cha kule ambako wafanyabiashara wetu wanakutana, kwenye mipaka yetu, na miji mikubwa kama Dar es Salaam ambapo biashara ndiko inapoanzia kuja huku Zambia.

Tupo tayari kuiwezesha Tanzania kuwahudumia ndugu zetu ambao hawakubarikiwa na Mwenyenzi Mungu kuwa na bandari kwenye nchi zao, ameeleza Waziri Kijaji.

Amebainisha kuwa “Marais wetu walikubaliana kuondokana na vikwazo visivyo vya kikodi na hata vile vya kikodi tushughulike navyo kwenye vikao vyetu vya kitaalamu hadi ngazi ya Mawaziri na tuondokane kabisa na vikwazo vyovyote vya kiabiashara, dhamira ikiwa ni kuongeza biashara kati ya nchi hizo mbili.”

Akizungumzia hatua zinazoendelea kufanyika katika kuweka mazingira bora amesema tangu Agosti mwaka jana baada ya Rais Hichilema kutembelea Tanzania mawaziri wa kisekta wameshakutana mara kadhaa na wameondoa baadhi ya vikwazo visivyo vya kikodi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter