Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema bidhaa zote nchini zitapanda bei.
Amesema kuwa mabadiliko ya kupanda bei za bidhaa yanatatokana na kupanda bei ya mafuta duniani ambapo imechangiwa na vita inayoendelea kati ya Russia na Ukraine.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika viwanja vya Maisara, Zanzibar Rais Samia amesema Tanzania itaathirika kwa bei ya bidhaa kupanda.
“Tanzania haitanusurika kutokana na kupanda bei ya mafuta kutokana na vita inayoendelea Ukraine na Urusi.
Tumeanza kusikia minong’ono huko, maisha yanakuwa magumu, kila kitu kinapanda bei, hao viongozi wetu tulionao hawana baraka hawana nini, si baraka ya viongozi ni hali ya ulimwengu inavyokwenda , mafuta yanapanda bei duniani na bidhaa zote zitapanda bei”, amesema Rais Samia.
Mwishoni mwa mwezi Februari Wizara ya Nishati ilitangaza kuondoa tozo ya Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu kuanzia mwezi Machi.
Taarifa ya Wizara ilisema kuwa sababu za kuondoa tozo hiyo ni kutokana na kuendelea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo vita kati ya Russia na Ukraine.