Kufatia zama za kidijitali wafanyabiashara duniani wametakiwa kwenda sawa na mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kuendesha biashara zao katika mifumo ya kisasa ikiwa ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi . Inaelezwa kuwa hadi kufika mwaka huu kuna watumiaji takribani bilioni 4 wa intaneti hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa kila biashara kuwa na tovuti(website) ili kuweza kutoa taarifa zaidi kuhusu huduma na bidhaa wanazouza.
Mbali na kuwa na tovuti ya biashara, muundo wa tovuti husika ni muhimu sana kwani utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya 70% ya watu huunda maoni yao kuhusu tovuti kutokana na muundo wake, hivyo hiyo inaweza kuwahamasisha kujua zaidi machapisho yaliyopo katika tovuti hiyo au kutokujihusisha nayo.
Hivi hapa ni vidokezo saba ambavyo vinaweza kukusaidia kujua vipengele ambavyo mteja wako atatarajia, au kutaka kuona katika tovuti yako ya biashara:
- Rahisisha mchakato mzima wa kufika katika tovuti yako. Epuka kuweka kurasa nyingi zisizo na maana,ili iwe rahisi kwa mteja kubofya tovuti yako kwa urahisi na hata kubofya kwa urahisi nyaraka zilizopo ndani ya tovuti yako. Hivyo inapofika katika suala la ‘Navigation’ unda mpangilio ambao ni rahisi kuelewa.
- Kwa kawaida kila tovuti hutengenezwa kwaajili ya malengo maalum, ikiwa tovuti yako imeundwa kwaajili ya kutoa habari,kuuza, kuuliza maswali nk ni muhimu sana kuweka sehemu maalum ya kubonyeza kwa urahisi ‘call to action’ ili kuweza kufikia taarifa husika. Kwamfano unaweza kutumia amri kama ‘ Nunua sasa’ ‘jisajili hapa’ na nyingine nyingi kutokana na maudhui yaliyopo .
- Picha na video huvutia zaidi wateja. Na wengi hununua bidhaa au huduma kutokana na maudhui ambayo huonekana katika picha na video. Hivyo katika tovuti yako tumia video na picha kuelezea zaidi biashara yako ikiwa ni pamoja na kuweka mirejesho, na ushuhuda kutoka kwa wateja wengine. Mbali na hayo hakikisha bango(banner) linaloelezea kuhusu bidhaa au huduma unayotoa linavutia, kwani bango hilo litaeleza kila kitu kuhusu biashara yako katika picha au video moja, pindi mteja anapofungua tu tovuti husika.
- Kipengele cha mawasiliano ni kipengele muhimu kinachotakiwa kuwepo katika tovuti yako. Inaleta urahisi ikiwa mteja anataka kukufikia aidha kwaajili ya kununua au kujua habari zaidi. Hakikisha mchakato mzima wa mawasiliano ni rahisi ili kuepuka kupoteza wateja hasa wapya.
- Inaweza kuwa Facebook, instagram, LinkedIn, Pinterest na nyingine nyingi lakini biashara nyingi siku hizi zipo katika mitandao ya kijamii. Ikiwa unatoa huduma au kuuza bidhaa ambayo inawavutia watu wengi, inashauriwa kukuza wigo wako wa mashabiki kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii. Hii itarahisisha kufikisha habari kuhusu biashara yako kwa wateja wa zamani na hata wapya wanaotumia mitandao hiyo. Sio lazima kuweka linki za mitandao yako ya kijamii lakini hata kuweka nendo za mitandao ya kijamii unayotumia ni habari tosha kwa mteja kujua majukwaa mengine ambayo anaweza kupata habari zaidi kuhusu biashara yako.
Aidha, kama wewe ni mtaalam katika tasnia yako si vibaya kuandika uzoefu na misingi unayoijua kuhusu tasnia husika. tenga muda maalum wa kuandika, si vibaya kuwauliza wateja masuala ambayo wangependela kujifunza zaidi na mwisho tengeneza utamaduni maalum wa kuchapisha katika tovuti yako, hii itakusaidia kuongeza trafiki katika tovuti yako na hata kupata wateja wapya.