Mitandao ya kijamii ni fursa nzuri kwa mfanyabiashara kujitangaza, kukuza biashara na vilevile kuwasiliana moja kwa moja na wateja. Japokuwa mitandao kama Facebook na Instagram ni ngazi kubwa ya mafanikio, kuna wafanyabiashara ambao wamejikuta wakikosa soko na kufilisika kutokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Kama mfanyabiashara, ni muhimu kutambua kuwa wewe ni sehemu ya maisha ya kila siku ya wateja wako hivyo unapaswa kuhakikisha kuwa vitendo au maoni yako binafsi kuhus jambo fulani haviathiri biashara yako kwa namna yoyote.
Unapotumia mitandao ya kijamii, epuka yafuatayo:
- Siasa na Dini
Mara nyingi maoni binafsi kuhusu siasa au dini huwa chanzo cha kutoelewana kwa sababu ni mada ambazo kila mtu huwa na imani/mawazo tofauti. Kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, ni muhimu kuepuka kuweka maoni yako binafsi kuhusu vitu hivi kwenye mitandao ya kijamii kwani unaweza kujikuta umepoteza wateja kutokana na utofauti huo.
Hii haimaanishi kuwa unanyimwa haki ya msingi ya kila binadamu kuwa na maoni yake. Kwa sababu wateja wako ni watu wa aina mbalimbali, ni vizuri kuepuka mada ambazo zinaweza kuwafanya wajisikie kama wanatengwa. Wekeza nguvu kubwa kwenye kuzungumzia masuala ya biashara, kusikiliza maoni ya wateja n.k. Mitandao isiwe sehemu ya kuzungumzia masuala na siasa wa dini.
- Kurudia kitu kimoja kila wakati
Hakuna mtu ambaye anapenda kuona kitu kimoja mara zote. Fikiria kama wewe ni mtumiaji wa Instagram na kila siku, kuna akaunti fulani inazungumzia ofa tu. Bila shaka baada ya muda mfupi utachoka kwa sababu hakuna kitu kipya kinachozungumziwa. Hivi ndivyo ilivyo kwa wajasiriamali mitandaoni, kama unafanya biashara ya viatu, haimaanishi kuwa unatakiwa kuzungumzia viatu vyako kila siku. Badilisha na wape wateja wako kitu tofauti bila kuwapoteza. Kwa mfano, unaweza kuwapongeza wateja walionunua viatu, unaweza kuonyesha aina nyingine ya viatu, unaweza kutoa ushauri wa namna ya kutunza viatu n.k.
- Kuzungumza mabaya
Wateja hawatembelei ukurasa wako ili kukutana na habari za mambo mabaya. Wanatembelea ili kukutana na kitu ambacho kitawaburudisha na kuwavutia. Kwa mjasiriamali, unapoanza kuzungumzia mambo mabaya yanayoendelea kwenye maisha yako binafsi, kwenye biashara au kwenye jamii inayokuzunguka, huduma au bidhaa yako ni rahisi kusahaulika. Licha ya kusahau kuhusu biashara, wateja wengine wanaweza kuachana na ukurasa wako kutokana na maudhui hayo. Kama umekosa jambo zuri la kusema kuhusu kitu fulani, ni vizuri kuachana nalo na kuhakikisha halifiki mitandaoni.
- Kuweka vitu vingi kwa wakati mmoja
Mitandao kama Facebook na Instagram ni sehemu kubwa ya maisha ya watu, wakiwemo wafanyabiashara. Japokuwa matangazo ni muhimu, ni vizuri kuwa na ratiba maalum ili kutangaza bidhaa zako kwa mpangilio maalum. Ukiweka vitu vingi kwa wakati mmoja, mteja anaweza kuona kama ukurasa wako ni kero na kuachana nao. Jitangaze kwa mpangilio maalum.
- Kusambaza taarifa zisizo rasmi
Katika ulimwengu huu wa mitandao, epuka kusambaza taarifa za uongo/usizoweza kuthibitisha kwani kufanya hivyo kutasababisha wateja wako kukosa imani na wewe pamoja na biashara yako kwa ujumla. Hakikisha taarifa zako ni za uhakika na kwamba umefanya utafiti kabla ya kuzichapisha mtandaoni.