Home BIASHARA Vodacom yazindua mtandao wa 4G visiwani Zanzibar

Vodacom yazindua mtandao wa 4G visiwani Zanzibar

0 comment 105 views

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc imezindua huduma ya intaneti yenye kasi ya 4G visiwani Zanzibar(Pemba na Unguja),ambapo wakazi wa visiwa hivyo sasa watapata fursa ya kipekee kufurahia mtandao wenye kasi zaidi nchini.

Katika visiwa hivyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc ina minara zaidi ya 53 yenye kasi ya 4G, 3G na 2G ambayo inawezesha wakazi hao kufurahia huduma kutokana na uwezo wa vifaa vyao.

Akizungumza juu ya maendeleo hayo, Mkurugenzi wa kitengo cha Network wa Vodacom, Alec Mulonga alisisitizia kwamba, kampuni hiyo imejikita katika kuipeleka Tanzania kwenye zama za kidijitali na kuhakisha kwamba kila mtu anaunganishwa.

“Vodacom Tanzania inaamini katika nguvu ya teknolojia kwenye kuleta maendeleo na kutoa fursa mpya. Kuunganisha ngome hii ya utalii – Zanzibar na huduma yetu ya 4G kutaleta fursa mpya za maendeleo kwani tutakuwa tumeifungua katika soko la dunia na huduma nyingine za kimtandao kama elimu, afya, kilimo na usalama pamoja na kukuza uchumi wa Wazanzibari,” alisema Mulonga.

Uwepo wa intaneti umebadilisha namna ya upatikanaji wa taarifa na ufanyaji biashara. Na kwa upande wa utalii, intaneti inauwezo wa kuwafanya watalii kufurahia zaidi safari zao nchini Tanzania na vile vile kuwaongezea uwezo wa kupata huduma za malazi kwa gharama nafuu kupitia mtandao.  Pia ni chombo cha kuwezesha utangazaji wa biashara na mawasiliano kati ya watoa huduma na watu wengine.

Kwa zaidi ya miaka 20, Vodacom Tanzania imewekeza katika kuboresha mtandao wao ili uweze kuwafikia na kuwaunganisha mamilioni ya Watanzania. Upatikanaji huu wa mtandao wenye kasi utawezesha ufanisi wa utendaji kazi wa sekta ya utalii visiwani Zanzibar.

Kwa sasa, kampuni inajivunia kutoa huduma za kimtandao kwa asilimia 90% ya idadi ya watu nchini Tanzania, ikiwa inamiliki zaidi ya minara 3000 ya 2G, 2500 ya 3G na 1000 ya 4G, kati ya hiyo minara 57 ikiwa ya 4G+ ambayo hutoa mtandao wenye kasi kuliko zote hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwanakheri Abdulswamadu, mkazi wa Mchambawima Unguja alieleza furaha yake kuhusu upatikanaji wa mtandao huo wenye kasi zaidi, “Ninafanya biashara na nina wateja ambao wako katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, na hivyo kupitia mtandao huu wenye kasi itakuwa rahisi kwangu kuwasiliana nao na kuwashawishi kununua bidhaa zangu.”

“Tunachokiona leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Vodacom Tanzania kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa mtandao wetu, Mfano; mwaka uliopita tuliingia mkataba wa kukodisha mkongo wa Taifa (NICTBB) na kuboresha vituo vyetu kote nchini. Tumedhamiria kuwekeza kwenye miundombinu ya mtandao ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu upande mawasiliano na pia kupunguza utofauti wa kidijitali, pia kuimarisha uwezo wa ushindani kati ya mashirika ya mawasiliano hapa nchini,” alihitimisha Mulonga.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter