Ofisa Madini Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda, amesema baada kufunguliwa rasmi kwa soko kuu la dhahabu mkoani humo, kumekuwa na mwitikio mzuri wa wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao tayari wameshaanza kuuza madini hayo katika soko hilo. Ikiwa zimepita siku kumi tu tangu soko hilo kuzinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mapunda amesema tayari ameshafanya mazungumzo kwa njia ya simu na wanunuzi kutoka nchi za nje kama Oman na Zimbabwe.
“Mbali na kupokea simu za wanunuzi wa dhahabu kutoka nje ya nchi, pia nimewapokea wageni wa kichina ambao nao wanataka tuwapatie ofisi ndani ya soko ili waanze kununua madini, tumejipanga kuwahudumia vizuri wageni ili waweze kufikiria matarajio yao”. Amesema Mapunda.
Ili kutatua malalamiko ya wachimbaji kuhusu ukosefu wa masoko ya madini yao sababu ya utoroshwaji nchi za nje, serikali iliamua kila mkoa uanzishe soko la madini illi wachimbaji waweze kuuza madini yao na kunufaika. Mkoa wa geita umekuwa wa kwanza kuanzisha soko la madini na sasa wachimbaji wanne hadi watano kila siku wamekuwa wakifika katika soko hilo kuuza madini yao.