Home BIASHARA Wafanyabiashara mtandaoni watakiwa kujisajili

Wafanyabiashara mtandaoni watakiwa kujisajili

0 comment 152 views

Wafanyabiashara kwa njia ya mtandao (kidigitali) sasa wametakiwa kujisaliji ili kurasimisha biashara zao na kuingizia serikali mapato kwa njia ya ulipaji kodi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka watu wote wanaofanya biashara kwa njia ya mtandao kufika kwenye ofisi zao kujisaliji na kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN).

Akizungumza katika kituo cha redio , Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Richard Kayombo amesema “wapo watu ambao hawajajisajili, wamehifadhi mizigo sehemu Fulani hawa tunawapa wito wajitokeze wajisajili ili waweze kulipa kodi kama wafanyabiashara wengine”.

“Sheria inaagiza kuwa siku 15 baada ya kuanza kufanya biashara, unatakiwa uje mwenyewe ujisajili upewe TIN uanze kulipa kodi kwa sababu ni biashara kama biashara nyingine,” ameeleza Kayombo.

Amesema TRA inatambua kuwa kuna watu kwa sababu mbalimbali wanaweza wakaamua wasiwe na duka kwa kukwepa gharama za kupanga na wanawashauri wajitokeze wawe sehemu ya walipa kodi.

“Kufanya biashara bila kujisajili maana yake ni moja kwa moja kuwa unakwepa kodi, na kingine ni kuleta ushindani usio na haki kati yake na wafanyabiashara halali ambao wamejisajili na wanalipa kodi.

Changamoto nyingine kwa upande wa kwake endapo atapata kazi ya kuuzia kampuni au taasisi kama hajajisajili hataweza kufanya hivyo kwa sababu hatakuwa na nyaraka zinazomuwezesha kufanya kazi na kampuni au taasisi na hata akihitaji mkopo kutoka katika taasisi za kifedha hatokuwa na nyaraka zinazomtambulisha”.

Ametoa wito kwa wale wote wanaofanyabiashara kwa njia ya mtandao na hawajajisajili wajitokeze waweze kuchangia mapato ya serikali.

“Mtu anajitangaza nauza bidhaa fulani bei zake ni hizi anakuuzia ina maana hatakupa risiti, sasa bidhaa ile ikiwa na tatizo wewe utadhibitishaji kwamba umenunua kwa Fulani wakati hata mahali anapouzia au makzai yake hujui?.

Ndio maana tunasisitiza kwa nia njema kabisa kwamba biashara inayofanyika mtandaoni ni biashara kama nyingine yeyote na inastahili kusajiliwa.”

Ameeleza kuwa kumekuwa na kesi nyingi za kutapeliwa kwenye biashara ya mtandaoni ambapo baadhi ya watu wanakwambia lipa nusu alafu mzigo nitakuletea na mxigo haufiki.

“Kujisajili kuataepusha wananchi na mambo ya kutapeliwa lakini vilevile kutawezesha wafanyabiashara kuchangia kodi na kutambulika”.

Amefafanua kuwa sheria ya mapato nchini inasema mtu ambae anapata mapato yanayofikia milioni nne na kuendelea kwa mwaka anatakiwa asajiliwe apata TIN na awe sehemu ya mlipa kodi.

“Bahati nzuri viwango vya kulipa kodi kwa mtu mwenye milioni nne hadi saba kwa mwaka ni kama laki moja,” amesema Kayombo.

“Naomba niondoe upotoshaji unaoenezwa kwamba ni biashara zinazoanza, sio wanaofanya biashara mtandaoni ni wanaoanza peke yao, kama hajafika milioni nne na hana uhakika wa wateja hastahili kulipa kodi, na hakuna atakae mgusa, tunaowazungumzia ni yule ambae mauzo yake yamefika milioni nne na kuendelea kwa mwaka anatakiwa ajisajili na kulipa kodi,”

Amesema sio kweli kwamba wanaofanya biashara kwa njia ya mtandao ni wafanyabiashara wadogo pekee bali ni biashara kubwa, za kati na ndogo.

“Tunachofanya tunatekeleza kile kinachohitajika, kwa weledi lazima tuwape wito waje wenyewe, sio kwa kuwafata, kuwafata ni hatua nyingine kwamba umekaidi, ndio maana tunatoa wito mtu asiseme hajawahi kuambiwa,” ameeleza Kayombo.

Wafanyabiashara wengi wanatumia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instagram na Youtube kutangaza biashara zao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter