Wakati akitembelea kiwanda cha sukari na shamba la miwa lililopo gereza la Mbigiri mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amesema anazo taarifa za wafanyabiashara wakubwa kuingiza maslahi binafsi kwenye miradi inayoendeshwa na serikali.
“Kuna taarifa za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari kupenyeza maslahi yao binafsi katika miradi hii mikubwa ya serikali ikiwamo shamba hili la miwa hapa Mbigiri, nawaasa waache mara moja kwa kuwa watakapobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kosa la uhujumu uchumi”. Ameeleza Naibu Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa serikali imelenga kukuza viwanda nchini ikiwamo kiwanda hicho ili wananchi waweze kujipatia ajira na kukuza uchumi wa taifa. Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Mbigiri, ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Magereza, Shija Fungwe amesema wana mpango wa kulima hekta 700 hadi kufikia Juni mwaka huu na kwamba hadi sasa, hekta 200 kati ya 500 tayari zimeshalimwa.