Na Mwandishi wetu
Wafanyabiashara wadogo wadogo katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma kwenye eneo la Ubungo mataa jijini Dar es salaam wametakiwa kuondoka katika maeneo hayo wao wenyewe hadi kufikia siku ya jumapili ili kuruhusu ujenzi wa mradi wa barabara za juu maarufu kama Fly over.
Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob baada ya kuzungumza na wamachinga hao amesema waanze kuondoka ifikapo jumamosi na kwamba manispaa hiyo imetenga eneo kubwa la wafanyabiashara karibu 5,000 katika kituo cha mabasi cha Mawasiliano hivyo shughuli zao za kibiashara zitaendelea kama kawaida.
Mbali na kuwasihi wafanyabiashara kuhama katika eneo hilo, Jacob pia ametumia fursa hiyo kutangaza nafasi mbalimbali za ajira zitakazopatikana pindi mradi huo unaotegemea kuwa na wafanyakazi na vibarua zaidi ya 5,000.
Mradi wa barabara za juu wa Ubungo unategemea kuanza muda wowote na utajengwa na Kampuni ya CCECC kutoka China kwa gharama ya Sh. 188.7 bilioni ambapo Benki ya dunia itatoa Sh. 186.8 bilioni kati na hizo huku serikali ikitoa Sh. 1.9 bilioni za usanifu mradi.