Home BIASHARA Watanzania watakiwa kuchangamkia fursa Zambia

Watanzania watakiwa kuchangamkia fursa Zambia

0 comment 345 views

Watanzania wametakiwa kujiandaa kuchangamkia fursa za masoko nchini Zambia kwa bidhaa za chakula hasa nafaka, nishati, uchukuzi, mavazi, vyombo vya nyumbani, vipodozi, vinywaji vikali na uwekezaji wa kibenki.

Balozi wa Tanzania nchini Zambia Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule ameeleza hayo wakati wa Kikao cha Kwanza kwa njia ya mtandao cha maandalizi ya ziara inayoratibiwa na TanTrade ya kufanya utafiti wa masoko na kutafuta fursa zilizopo nchini Zambia inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 hadi 28 Aprili, 2023 katika Jiji la Lusaka Zambia.

Balozi Mkigule amesema fursa ya kuuza chakula ipo katika maeneo ya mahoteli yaliyopo katika mji wa Livingstone hasa mchele, soya na maharage. Pia, kuna fursa ya kuuza mavazi ya vitenge, vikoi, mabegi, nywele bandia, mafuta ya nywele na manukato.

Ameongeza kuwa kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika huduma za kibenki ambapo wafanyabiashara wengi Watanzania nchini humo wanakosa huduma za kibenki za Tanzania na hivyo hulazimika kurudi Tanzania ili kuweka fedha.

“Watanzania wengi wanaofanya biashara hapa ni wateja wa benki za NBC, NMB na CRDB ambao wanalazika kukusanya fedha kwa kipindi fulani na baadae hulazimika kurudi Tanzania kuziweka katika benki hizo,” amesema.

Amesema “hii ni fursa kwa benki zetu za NBC, NMB na CRDB zianze mikakati ya kuwekeza katika hapa kwani Watanzania ni wengi wanaohitaji huduma za kibenki”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TanTrade kuanza kufanya tafiti na intelijensia ya masoko ambapo tayari utafiti umefanyika Nchini Sudan ya Kusini na tafiti nyingine zinatarajiwa kufanyika kwa nchi za Zambia, Malawi na Rwanda.

Amemshukuru Balozi Mkigule kwa jinsi anavyoshirikiana na TanTrade katika kutafuta masoko ya nje ya bidhaa za Tanzania na taarifa za awali alizotoa zitasaidia utafiti kufanyika kwa ufanisi na kuwa na matokeo tarajiwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter