Home BIASHARA ZIJUE BIASHARA ENDELEVU

ZIJUE BIASHARA ENDELEVU

0 comment 129 views

Mazao ya chakula
Biashara ya kununua na kuuza mazao ya chakula ni biashara nzuri ambayo ina faida kubwa na pia soko lake ni la uhakika kwa sababu kila mtu anahitaji chakula. Bei za mazao huwa zinabadilika mara kwa mara kufuatana na msimu. Kwa mfano; wakati wa mavuno mazao huwa na bei ndogo na kupatikana kwa wingi ubunifu ni kuhamisha kutoka huko kwenye wingi na kuyauza kwenye uhaba kwa faida kubwa. Au unaweza kununua kwa wingi na kuhifadhi hadi msimu wa uhaba nawe ukauza kwa faida kubwa. Biashara hii inahitaji uwe na mtaji pia na maghala ya kutunzia mazao hayo. Unapaswa kujifunza mbinu za kuhifadhi mazao kama vile kuweka dawa za kuua wadudu ili mazao yasiharibike. Unaweza ukaamua kuwa mkulima wa mazao, kuyalima na kuyauza au kununua mazao na kuyauza. Ni muhimu kufanya utafiti wa soko la mazao yako kabla ya kufanya biashara hii ili usije ukashindwa kuyauza.

Huduma za kitaalamu.
Biashara ya kutoa huduma za kitaalamu ni nzuri sana na ina mapato mazuri, inaweza kuleta utajiri na maisha bora. Ili ufanye biashara hii unapaswa kwanza kusomea taaluma husika kwa kiwango kinachohitajika na wahitaji au masoko. Taaluma ambazo zina malipo mazuri ni ufundi, ualimu, uanasheria, udaktari ufamasia, uhasibu na ufundi wa vifaa vya elektroniki. Unaweza kuanza kwa kuajiriwa kwenye ofisi inayotoa huduma ya fani yako ili upate uzoefu na siri ya biashara hiyo. Kisha tafuta kuanza taratibu kufanya kazi zako binafsi. Ukiona biashara yako inaenda vizuri acha kazi na uende kufanya biashara yako kwa juhudi na maarifa yako yote na utafanikiwa.

Magari ya usafirishaji.
Biashara ya usafirishaji ni biashara pana sana ambayo inajumuisha magari ya abiria na magari ya mizigo. Ni biashara yenye faida sana, inayohitaji mtaji mkubwa na usimamizi wa hali ya juu ili kudhibiti wizi wa mapato. Kwa kuwa biashara hii ni pana kila aina ya biashara tutaizungumzia hapa nchini.

Kusafirisha abiria Dala dala
Biashara hii ni nzuri na inayo mapato mazuri ya uhakika. Ili uweze kufanikiwa katika biashara hii unatakiwa ununue gari ambalo ni zima. Usimamie kwa karibu na kudhibiti mapato ili yasiibiwe. Gari linatakiwa lifanyiwe ukarabati mara kwa mara ili liwe katika hali nzuri ya kufanya kazi. Uweke akiba nusu ya mapato ili kukabiliana na dharura ya matengenezo makubwa. Niliwahi kuzungumza na aliyekuwa mmiliki mmoja wa magari ya kusafirishia abiria dala dala kuhusu suala hili ambapo alisimulia mkasa uliomkuta. Yeye alikuwa analetewa mapato yake katika kumbi za starehe na kutumia hizo fedha, kunywea pombe. Alikuwa haweki akiba. Siku moja gari liliharibika na lilihitaji matengenezo ya Tshs 900,000/=. Mmliki huyo wa magari ya kusafirishia abiria alikuwa hana fedha hivyo aliamua kuuza gari. Matatizo ya aina hii ya biashara ni kuwapo watu wengi wanaotegemea kuchota mapato hayo nao ni dereva, kondakta, mawakala na kadhalika. Pia kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na dereva na kondakta kwa kusingizia kuwa gari limeharibika au limekamatwa na askari wa usalama barabarani wakati siyo kweli ili mapato wayaibe. Pia kuna wizi wa mafuta na vipuri. Ili kukabiliana na matatizo haya unaweza kumwekea kiwango maalum cha mapato anayopaswa kuwasilisha na dereva na kondakta. Kwa mfano, kwa gari la uwezo wa kubeba abiria 18 kiasi cha mapato ni Tshs 25,000/= kwa siku na gari la abiria 26 mapato ni Tshs 40,000/= kwa siku. Pia unapaswa kufuatilia nyendo za wafanyakazi hao. Unaweza kuingia mikataba na makampuni ya kusafirisha wafanyakazi au wanafunzi ili upate mapato ya uhakika pia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter