Kumbuka wiki chache zilizopita mambo hayakua kama yalivyokuwa sasa katika nchi mbali mbali duniani. Katika masoko na maduka ya jumla. Kinyume na awali maduka na masoko ya bidhaa kwa sasa utakuta vitakasa mikono au maji na sabuni ya kunawa mikono ili kujiepusha na maambukizi ya virusi vya corona.
Maafisa sasa wanashauri watu wapunguze safari za kwenda kununua bidhaa sokoni na katika maduka ya jumla kama njia ya kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya virusi.
Lakini je njia salama za kununua chakula au kukubali chakula cha kuagizwa na kuletewa nyumbani ni zipi?
Ni zipi hatari unazoweza kuzipata katika maduka ?
Coronavirus husambaa wakati mtu mwenye maambukizi anapokohoa na kutoa matone ya mate yenye virusi kwenda hewani. Hii inaweza kusababisha maambukizi iwapo mtu aliye karibu atavuta hewa yenye virusi hivyo au iwapo matone hayo yataangukia mahali na mtu mwingine kuyagusa na hatimaye kugusa uso wake.
Kwahiyo kwenda madukani au sokoni na kuchangamana na watu wengine ni jambo linalokuweka hatarini. Hii ndio maana agizo la watu kutokaribiana na walau kuwa mita mbili mbali na mtu mwingine -ni muhimu sana, kama maduka mengi ya jumla ya bidhaa yanavyosisitiza.
Maduka ya jumla yanaweza kusaidia “kuweka mfumo ” wa jinsi ya kudhibiti virusi vinavyosambaa anasema Profesa Sally wa taasisi ya London School of Hygiene and Tropical Medicine. “Watu wengi wanagusa na kurudisha bidhaa, wanatumia kadi za ununuzi za benki, pamoja na ATM, tiketi za malipo ya kuegesha magari, karatasi za hundi za malipo nakadhalika … bila kusahau ukaribu wa watu kadhaa katika maeneo hayo .”
Kuna njia za kuondokana na hatari hizi:
- Nawa mikono kwa sekunde 20 kwa sabuni na maji, au tumia vitakasa mikono(hand sanitizer) kabla na baada ya kununua bidhaa.
- Uchukulie maeneo yote kuwa si salama na yenye uwezekano wa kuwa na virusi vya corona, ikimaanisha kuwa epuka kugusa uso wako baada ya kutumia toroli za maduka ya jumla( supermarkets), vikapu, maboksi, mifuko na vitu vingine vya kubebea mizigo ya bidhaa.
Vipi kuhusu ununuaji wa bidhaa zenyewe?
Hakuna ushahidi kwamba Covid-19 inasambazwa kwa njia ya chakula, na kwamba kupikwa kwa chakula kunaweza kuua virusi.
Lakini huku kukiwa hakuna ushahidi kuwa “huwezi kupata hatari ya maambukizi kabisa “, anasema Profesa Bloomfield, jambo linalotia hofu zaidi ni suala la kufungwa kwa chakula na watu wengine ambao huenda wakawa na virusi.
Ushauri wa biashara za ununuzi wa bidhaa za mtandaoni : “Ufungaji wa chakula haujafahamika kusababisha .” Hatahivyo , baadhi ya wataalamu huru wana ushauri zaidi.
“Kwa bidhaa zilizofungwa kwenye kontena,” anasema Profesa Bloomfield, ” vinapaswa kuwekwa kwa saa 72 kabla ya kutumia
“Kwa bidhaa ambazo hazijafungwa, ambazo zinaweza kuwa zimeguswa na mtu mwingine – zioshe vizuri kwa maji yanayotiririka na uziache zikauke anasema.
Je vyakula unavyoagiza nyumbani ni salama kiasi gani ?
Bidhaa za vyakula vinavyoagizwa na kuletwa hadi nyumbani kwako vina hatari kidogo kwani utakua umeepuka safari ya kwenda kuvinunua katika maduka ya jumla na sokoni ambako unachangamana na watu wengi. Hata hivyo hatari iliyopo ni uwezekano wa vyakula hivyo kupata virusi mahali vilipowekwa wakati vinafungwa au kutoka kwa dereva aliyevileta kwako.
Mtaalamu wa usalama wa chakula na mwanablogi Dkt Lisa Ackerley anasema kuepuka hatari ya maambukizi ni vema kuacha ujumbe mbele ya mlango ukimueleza dereva anayeleta vyakula apige kengele na kurudi nyuma . Hii inakuwezesha kuchukua chakula chako kwa usalama, peke yako.
Profesa Alison Sinclair, mtaalamu wa virusi kutoka chuo kikuu cha Sussex, anaongeza kuwa : “Hazipaswi kuwepo hatari zaidi kutokana na uagizaji bidhaa kwa njia ya mtandao kuliko kuhudumiwa na rafiki au mtu anayejitolea kukusaidia kununua bidhaa kutoka sokoni au madukani .”
Baadhi ya wataalamu pia wanashauri utumie mfuko wa plastiki mara moja tu kubebea bidhaa na kasha uutupe wakati huu wa mlipuko wa coronavirus
Vipi kuhusu uagizaji wa vyakula vilivyopikwa?
Kwa sasa migahawa mingi imeshauriwa kuwafungia wanunuaji wa vyakula wakavile nyumbani.
Hatari ya vyakula vya aina hii huenda ikapunguzwa iwapo watazingatia usafi , anashauri Profesa Bloomfield, kuwa “mlaji kuweka chakula alicholetewa katika vyombo visafi, kutupa mifuko iliyotumiwa kubeba chakula na kunawa mikono yako vyema kabla ya kula”.
“Toa chakula kwenye kontena ulimoletewa kwa kutumia kijiko na ukile kwa uma na na kisu au kijiko- usile kwa kutumia kiganja na vidole vyako .
“Ni vyema zaidi katika hali tuliyonayo kwa sasa kuagiza vyakula vya moto vilivyopikwa muda huo huo, kuliko vyakula baridi au vibichi.