Visa vilivyokwisha thibitishwa duniani kote vya COVID-19 vinakaribia kufikia milioni moja, huku mtoto mchanga wa umri wa wiki sita akigundulika kuambukizwa virusi hivyo nchini Marekani.
Nusu ya ulimwengu mzima uko katika aina fulani ya kifungo kwa hivi sasa, mnamo wakati serikali zikihangaika kupunguza kasi ya kirusi cha corona ambacho tayari kimeua maelfu ya watu. Hatua hizo ambazo ni muhimu kwa ajili ya afya, zinatajwa na wataalamu kwamba zitasababisha uhaba mkubwa wa chakula duniani, kutokana na kwamba ugavi wa chakula umepungua na watu kufanya manunuzi kutokana na hofu.
Vifo vya COVID-19 vimeendelea kuongezeka, ambapo hadi sasa zaidi ya watu 46,000 duniani kote wamepoteza maisha. Marekani ambayo kwa hivi sasa inahesabika kuwa na karibu robo tatu ya maambukizi duniani kote, imeripoti vifo 5000 kulingana na chuo kikuu cha Johns Hopkins. Rais Donald Trump amesema mambo yatakuwa mabaya zaidi.
“Kama nilivyosema jana, siku ngumu ziko mbele yetu. Tutakuwa na wiki kadhaa, hususan siku chache kuanzia sasa ambazo zitakuwa za kutisha. Lakini hata katika nyakati ngumu, wamarekani hawakati tamaa, hatupatwi na hofu, tunakuwa wamoja, tunavumilia na tutashinda”, amesema Trump.
Katika taarifa za hivi karibuni mtoto mwenye umri wa wiki sita aliyepelekwa hospitali ya Connecticut nchini Marekani, amegundulika kuambukizwa COVID-19. Virusi hivyo awali vilikuwa vikiwaathiri wazee na wale walio na matatizo mengine ya kiafya lakini idadi ya kesi za hivi karibuni zimedhihirisha kuwa COVID-19 inaweza kuathiri watu wa rika zote.
Kansela Angela Merkel amesema Ujerumani itapanua hatua za watu kuto sogeleana zilizoanzishwa mwezi uliopita ili kupunguza kasi ya maambukizi hadi Aprili 19, na kuongeza kuwa serikali itafanya tathmini mpya baada ya sikukuu ya pasaka. Ujerumani imefunga shule, maduka, migahawa, viwanja vya michezo huku makampuni makubwa yakisimamisha uzalishaji ingawa kesi za virusi vya corona sambamba na vifo bado vinaongezeka, zaidi alisema “itakuwa vibaya sana endapo tutaondoa vizuizi hivi mapema sana na kisha tuvirejeshe baadae. Hii ina maana kuwa lazima tuzuie kila kitu kutoka kwenye chungu na kuingia motoni, lakini lazima mambo yaendelee sasa”.
Uingereza na Ufaransa zote zimeripoti kiwango cha juu cha idadi ya vifo vya COVID-19 siku ya Jumatano, ingawa hapakuwa na ishara kuwa virusi hivyo vinaweza kuongezeka barani Ulaya. Uhispania yenyewe vifo vimepindukia 9,000 huku Italia vikipanda hadi 13,000. Ajira zipatazo 900,000 zimepotea nchini Uhispania tangu nchi hiyo ilipoanzisha hatua za kuifungia miji yake.