Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 25 mwaka huu.
Rais Samia maetoa wito huo akizungumza katika kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Hayati Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli katika uwanja wa Magufuli, Chato.
“Tuendelee kuelimishana na kuhamasishana kwa ajili ya kushiriki kwenye zoezi la kuweka anuani za makazi na baadae kushiriki mkwenye zoezi la sensa ya watu na baadae mwezi wa nane tuje tujitokeze kuhesabiwa,” Amesema Rais.
Amesema “jana nilikuwa na mkutano na ndugu zetu watu wenye ulemavu, tuna lengo la kuhesibiana kujua idadi yetu, lazima tujuane wanawake wangapi wanaume wangapi na ndugu zetu wenye ulemavu wako wangapi, niwaombe sana wananchi tusiwafiche, tutakapofika kuhesabiana kama kuna nyumba ina mtu mwenye ulemavu waseme.”
Aidha, Rais Samia amesema mema yote yaliyoachwa na Hayati John Magufuli yataendelezwa.