KAMPUNI ya magari ya AMC Tanzania imepeleka furaha shule ya Viziwi Buguruni baada ya kukabidhi uongozi wa shule bidhaa mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi 237 wanasoma katika shule hiyo.
Kampuni ya AMC Tanzania ndio wauzaji pekee wa magari aina ya Nissan nchini.
Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya AMC Tanzania, Christophe Henning amesema kwamba wamejisikia fahari kusaidia wenye mahitaji.
Aidha alisema kwamba kampuni yake itakaa katika meza tena na uongozi wa shule hiyo kuona namna ya kuisaidia shule hiyo.
Kampuni ya AMC TANZANIA ambayo kwa sasa inatimiza miaka mitano tangu kufunguliwa nchini imesema kwamba inafanya hisani hiyo kurejesha faida kwa wananchi.
“Kama sehemu ya wajibu wetu wa kurejesha faida kwa wananchi tumeona tujikite kusaidia wenye mahitaji hasa watoto ili waweze kupata elimu katika maizngira bora kwani tunaamini viwili (watoto na elimu) hivyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi.” alisema Henning.
Kampuni hiyo miongoni mwa bidhaa walizowapa wanafunzi ni mabegi na kompasi.
Alisema kwamba kampuni ya Nissan ambayo inatengeneza mitambo mbalimbali inajivunia kauli mbiu yake ya ubunifu unaofurahishwa ambao umewafanya kuwa moja ya makampuni ya kutumainiwa duniani na yanayofanya biashara vyema.
Alisema kutokana na bishara zake wanapata nafasi ya kurejesha faida kwa jamii kwa kuwekeza zaidi kwa watoto wenye mahitaji na elimu yao.
Nissan ambao kwa sasa wapo Plot No. 6, Vingunguti Area, Nyerere Road na kuwa na matawi katika miji mikuu ya kibiashara nchini kama Arusha, Dodoma, Zanzibar, Mwanza, Mbeya na Morogoro.
Katika hotuba yake mtendaji huyo aliahidi Nissan Tanzania kuendeleza ushirikiano na shule ya Buguruni kwa manufaa ya pande zote mbili ili kuleta ustawi katika jamii.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Kulwa Milembe akishukuru kwa zawadi hizo alisema kwamba wanafunzi wake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo vifaa vya kubebea vitu wanafunzi ambao wengine wametoka nje ya Dar es salaam na familia zao ni duni sana.
Alisema wanafunzi wengi wamekuwa hawana vibebeo vya madaftari, kwa hiyo msaada wa mabegi ni tunu kubwa kwao.
Alisema pamoja na msaada huo atapenda kampuni hiyo kuendelea kusaidia wanafunzi wake ili waweze kusonga mbele katika elimu.
Shule hiyo yenye wavulana 110 na wasichana 127 na kufanya jumla yao kuwa 237 ina vitengo vya msingi, ufundi, awali na wasioona.