Serikali ya Tanzania imetenga kiasi cha Sh bilioni 48 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi 8,000 wa Stashahada (Diploma) katika mwaka wa masomo 2023/2024.
Hayo yamebainishwa Oktoba 4, 2023 na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda akieleza mchakato wa mikopo jijini Dar es Salaam.
Amezitaja fani za kipaumbele kuwa ni pamoja na afya na sayansi shirikishi, fizikia na masomo ya amali, ualimu wa hisabati, usafiri na usafirishaji, uhandisi na nishati, kilimo na maendeleo ya mifugo.
Amesema dirisha la kuomba mkopo litakuwa wazi kwa siku 15 kuanzia Oktoba saba hadi 22, 2023 na yatafanywa kwa njia ya mtandao.
“Muongozo huo utapatikana kuanzia leo, lakini wanafunzi, wazazi na walezi watumie siku nne kuusoma kabla ya kuanza kuomba, ni muhimu sana.
Unaweza ukaomba ukakosa unashangaa kwa sababu kipaumbele ulichokuwa unakiwinda ili upate mkopo umekikosea,” amesisitiza Waziri Mkenda.
Amebainisha kuwa baada ya kumaliza masomo mwanafunzi mnufaika atatakiwa kurejesha mkopo wake kwa kiwango cha asilimia 15 ya mshahara wake wa kila mwezi.