Home Featured Tanzania yakaribia kuwa taifa la uchumi wa kati

Tanzania yakaribia kuwa taifa la uchumi wa kati

0 comment 122 views

Ndoto ya Tanzania kuwa nchi ya uchumii wa kati ifikapo mwaka 2025 ipo karibu kutimia.

Hayo yalisemwa jana na Dkt. Tausi Mbaga Kida, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (Economic and Social Research Foundation- ESRF) katika semina iliyoandaliwa kwa pamoja baina ya taasisi hiyo na Benki ya Dunia kujadili safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa semina ya pamoja kati ya Benki ya Dunia na ESRF juu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika semina hiyo, Dkt. Tausi Kida alisema kuwa hadi kufikia sasa pato la wastani la mtanzania ni dola za kimarekani (USD) 910 wakati inahitajika kwa taifa kufikisha kiwango cha pato la wastani la USD 995 kuwa taifa la uchumi wa kati.

“We are almost there – tumekaribia kabisa kufika” Kinachotakiwa sasa ni kuzidisha juhudi ili kasi ya ukuaji wa uchumi usishuke bali izidi kuongezeka – alisema.

Ili kuifikia lengo hilo, Dkt. Tausi Kida alishauri pia kufanyika mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuongeza tija sambamba na kuongeza usindikaji wa mazao ya kilimo hii ikiwa ni katika jitihada za kuondokana na kilimo cha kujikimu na kujikita zaidi katika kilimo cha kibiashara chenye kulenga mahitaji ya soko la ndani na nje.

Sambamba na hilo, Dkt Tausi Kida alishauri pia kuongeza uwekezaji katika rasilimali watu hususani kuboresha upatikaji wa huduma za afya, elimu na maji kama njia ya uhakika ya kuondokana na umaskini ifikapo mwaka 2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Kida (kulia) akizungumzia umuhimu wa kuangalia rasilimali watu kwa kuzingatia weledi na elimu yao katika ushiriki wa kujenga uchumi wakati wa kujadili mada kwenye semina ya pamoja kati ya Benki ya Dunia na ESRF juu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

Akifafanua zaidi, Dkt Tausi Kida alieleza kwamba tangu mwaka 2000, Tanzania imekuwa ikitekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa (Development Vision 2025) inayolenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Dkt. Tausi Kida aliwaeleza washiriki wa semina kuwa dira hiyo imelenga kubadili uchumi wa Tanzania kutoka kutegemea sekta ya kilimo yenye tija ndogo na kuwa taifa lenye kutegemea zaidi uchumi wa viwanda na hasa viwanda vyenye kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kumudu ushindani wa soko la kimataifa.

Sehemu ya wadau wa maendeleo,sekta binafsi pamoja na taasisi mbalimbali za serikali waliohudhuria semina ya pamoja kati ya Benki ya Dunia na ESRF juu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

Akifafanua zaidi, Dkt Kida alisema kuwa Dira hii ya Maendeleo ya Taifa inalenga pia kuondoa kabisa umaskini nchini Tanzania ifikapo mwaka 2025. “It is envisioned that by 2025 abject poverty shall be something of the past – ni ndoto yetu kwamba ifikapo mwaka 2025 suala la umaskini litakuwa ni jambo lilipitwa na wakati nchini Tanzania” alisema.

Alieleza kwamba Tanzania imekuwa ikitekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa kupitia mikakati mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Kwanza na wa Pili wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini nchini Tanzania – mikakati ambayo ilifahamika zaidi kwa jina la MKUKUTA na Mipango ya Miaka mitano mitano ya Maendeleo ya Taifa ambapo kwa sasa taifa linatekeleza mpango wa pili kwa kipindi cha miaka ya 2016/17 – 2020/21 alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird alisema kwamba Benki ya Dunia itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania uliojengeka kwa zaidi ya miaka 54 sasa.

Ofisa Mtendaji Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bi Bella Bird akitoa neno la ufunguzi wa semina ya pamoja kati ya Benki ya Dunia na ESRF juu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

Ushirikiano huu unalenga kuiwezesha Tanzania kuwa moja ya mataifa yenye uchumi mkubwa duniani. Bi Bella aliuambia mkutano kwamba katika miaka hiyo yote, Benki ya Dunia imekuwa ikitoa misaada ya kifedha kwa Tanzania hasa kupitia Shirika lake la Kimataifa la Fedha (International Development Association – IDA) ambalo limekuwa likitoa misaada katika nyanja mbali mbali hususani afya, elimu, hifadhi ya jamii, maji, nishati, uchukuzi, miji, mazingira, sekta za fedha na utawala bora.

Semina hiyo ilifanyika jana, Jumatano tarehe 21 mwezi wa 3 mwaka 2019 katika ukumbi wa mkutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

Dhumuni kuu ya semina hiyo lilikuwa ni kujadili safari ya Tanzania katika kuelekea uchumi wa kati. Semina hiyo ilichagizwa na mada iliyotolewa na ndugu Yutaka Yoshino, mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia ambaye alitoa mada juu ya uzoefu wa mataifa ya Vietnam na Bangladesh katika kufanya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya viwanda ambapo yamefanikiwa kupiga hatua na kuwa mataiafa ya uchumi wa kati katika miaka ya hivi karibuni.

Mchumi wa Benki ya Dunia, Bw Yutaka Yoshino akitoa mada kuhusu safari ya Tanzania kuelekea uchumi kati wakati wa semina ya pamoja kati ya Benki ya Dunia na iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.

“Both countries were at the same level of per capita income as Tanzania in early 1990s – pato la wastani kwa mataifa haya lilikuwa sawa na lile la Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1990” alisema.

Baadhi ya mataifa ya Afrika yaliyofanikiwa kutoka katika kundi la nchi maskini zaidi duniani na kuwa mataifa yenye uchumi wa katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na Ghana, Nigeria, Sudan na Zambia.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter