Home FEDHABIMA JIFUNZE MACHACHE KUHUSU BIMA

JIFUNZE MACHACHE KUHUSU BIMA

0 comment 77 views

Bima sio neno geni miongoni mwetu. Ni jambo ambalo tumekuwa tukikumbana nalo katika maisha yetu ya kila siku. Licha ya hali hiyo, watu wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na suala hili. Watanzania wengi bado hawajajiunga na huduma hii kutokana tu na uelewa mdogo walionao juu ya masuala ya bima.

Kabla ya yote inapaswa kufahamu bima ni nini? Huu ni mpango au makubaliano maalumu ambapo endapo janga au hasara yoyote itatokea, mkata bima atapokea fidia ambayo itatokana na fedha atakayokuwa anachangia kwenye kampuni ya bima. Kila mwisho wa mwezi mkata bima huwasilisha fedha kwa kampuni ya bima. Makubaliano haya hulindwa kwa mujibu wa sheria. Hapa nchini kwetu, Sheria ya Bima ya mwaka 2009 ndiyo inayotumika zaidi.

Kuna aina mbalimbali za bima na baadhi ni kama bima ya gari, moto, maisha, meli, bidhaa zinazosafirishwa, nyumba, ndege, wizi, dhamana na bima ya afya. Bima zinazoongozwa kukatwa kwa wingi na mwananchi wa kawaida ni bima za afya, bima za magari na bima za nyumba. Makala hii itaelezea kwa undani aina kuu nne za bima ambazo kila mfanyabiashara  mdogo na wa kati anapaswa kuwa nazo.

ADVERTISEMENT

Kila mfanyabiashara anapaswa kuwa na bima ya vitendo vya wizi. Aina hii ya bima itamfidia mkata bima hii pale ambapo wizi wa mali zilizopo kwenye biashara yake utatokea. Bima hii ina umuhimu mkubwa kwa mfanyabiashara kwani inamuhakikishia usalama wa mali zake na endapo wizi utatokea hatosumbuka kutumia fedha za ziada ili kurudisha mali iliyopotea

Aina ya pili ya bima kwa mfanyabiashara ni bima  dhidi ya majanga ya moto. Tunasikia kila siku maduka makubwa yanapata hitilafu ya umeme na kusababisha moto hivyo mfanyabiashara kupoteza bidhaa zake zote. Bahati mbaya jambo hili likitokea, bima hii itagharamia hasara zitakazopatikana na kumsaidia mfanyabiashara kuendelea na kazi yake ambayo inawezekana asingeweza kuiendeleza bila ya kuwa na bima hii.

Aina ya tatu ni bima ya mali ambayo husaidia pale mfanyabiasha anaposafirisha mizigo kwa njia ya gari, treni, meli au ndege. Upotevu wa aina yoyote ukitokea wakati wa shughuli za usafirishaji, basi mfanyabiashara atapatiwa fidia. Na aina ya nne ni bima ya afya ambayo humuwezesha mtu kupata matibabu hospitalini tatizo la kiafya linapotokea.

Wanafanyabiashara wanatakiwa kujenga mazoea ya kuwa na huduma za bima kwani mi muhimu sana katika ukuaji na maendeleo ya biashara zao. Endapo watapatwa na majanga yoyote yale inakuwa rahisi kwa wao kupata fidia moja kwa moja kutoka katika kampuni husika za bima, na hivyo kuondokana na wasiwasi wa kutumia fedha nyingine ili kujikwamua.

Makampuni ya bima nayo yawe mstari wa mbele katika kuelimisha jamii hasa wafanyabiashara wadogo mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba watu wana uelewa wa kutosha juu ya huduma za bima pamoja na umuhimu wake.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter