Home FEDHABIMA Kampuni 10 bora za bima

Kampuni 10 bora za bima

0 comment 152 views

Bima ni muhimu kwa kila mtu, kwa sababu hakuna mtu ambaye hupanga janga litokee. Kwa mfano hivi sasa kumekuwa na mvua zisizoisha katika baadhi ya maeneo hasa jijini Dar es salaam na watu wengi wameathirika na mvua hizo kwa namna moja au nyingine.  Hivyo basi kama mtu ana bima basi inakuwa rahisi kutatua athari hizo kupitia bima.

Zipo kampuni nyingi zinazotoa bima za aina mbalimbali. Zifuatazo ni kampuni 10 zenye huduma nzuri zaidi:

ALLIANCE INSURANCE CORPORATION LTD

Kampuni hii wanatoa huduma za bima za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na bima ya moto, bima ya baharini, bima ya magari, bima ya uhandisi na nyingine nyingi. Kwa ujumla kampuni hii wameweka sera inayomruhusu mteja kupata bima ya kila aina hivyo ni rahisi kwa watu hasa wafanyabiashara kupata huduma ya bima ya aina yoyote.

AAR INSURANCE LIMITED

Hawa wamejikita katika utoaji wa bima za afya na uokoaji. Wanatoa huduma kwa watu binafsi na hata makampuni mengine au mashirika. Pia wana vifurushi mbalimbali ambavyo mteja anachagua kutokana na bajeti yake.

ICEA LION GENERAL INSURANCE COMPANY (T) LIMITED

Kampuni hii wana huduma ya bima za kila aina kwamfano wanatoa bima ya magari, bima ya makazi, bima ya kusafirisha mizigo, bima vifaa vya kielektroniki, bima ya mashine, bima ya ajali kwa wanafunzi, bima ya wafanyakazi, bima ya dhima (liability), bima ya ajali makazini (WIBA), na nyingine nyingi.

METROPOLITAN TANZANIA INSURANCE COMPANY LIMITED

Kwa ujumla kampuni hii inatoa huduma ya bima kwa umiliki wa vitu binafsi katika mali,moto, biashara, bima ya wizi, ajali za makundi au binafsi na hata bima katika kampuni. Pia hutoa vifurushi kuhusu wafanyakazi na mambo ya fidia, wakandarasi, masuala ya ujenzi wa hatari, matengenezo ya mitambo mizito na uingizaji wa mitambo hiyo, mizigo ya bandarini nk.

MILEMBE INSURANCE COMPANY LIMITED

Kampuni hii imelenga kutoa huduma za bima katika mambo binafsi na hata katika mashirika mbalimbali  ili kushughulikia hatari zozote zinazoweza kutokea. Wanatoa vifurushi vya bima mbalimbali ikiwa ni pamoja na  bima ya nyumba, wizi, vifaa, moto, uharibifu wa mashine, ajali binafsi, bima ya safari, bima ya usafirishaji wa mizigo, bima ya fedha, bima ya ajali binafsi na kadhalika.

MO ASSURANCE COMPANY LIMITED

Hawa wanajishughulisha zaidi na bima zinazohusiana na masuala ya bondi katika biashara na ujenzi. Kwa mfano wanatoa bima ya tetemeko la ardhi, moto, migomo, mafuriko, vitu vikidondoka kutoka angani, kukitokea na mlipuko na vifurushi vingine vingi. Pia wanatoa kifurushi cha upotevu wa fedha kutoka benki  au kwenda benki kama mtu atavamiwa na majambazi.

NATIONAL INSURANCE CORPORATION (T) LIMITED

Wanatoa huduma kwa mashirika, katika biashara, na hata kwa watu binafsi.  Bima hii ya taifa inatoa vifurushi vya maisha na visivyo vya maisha. Kama mteja atalipa bima ya maisha basi kampuni hii huhakikisha kuwa mteja anapata huduma stahiki ili mradi mteja huyo akiwa analipia fedha kulingana na makubaliano (Premium). Baadhi ya bima za maisha wanazotoa ni, bima ya moto, bima ya fedha, bima ya kuvamiwa, bima ya magari nk.

REAL INSURANCE TANZANIA LTD

Hawa wanatoa vifurushi vya huduma ya bima kwa mashirika makubwa, katika masuala ya wakandarasi, safari, magari, bima binafsi, bima ya baharini na bima kwa wajasiriamali.

SANLAM LIFE INSURANCE (T) LIMITED

Kampuni hii wanatoa huduma ya bima kwa watu binafsi, familia, na hata taasisi. Bima ya maisha katika kampuni hii inawahakikishia wanafamilia kuwa mambo yote yatakwenda sawa ikiwa mtu aliokata bima hii atafariki, pia wanatoa bima ya safari, bima ya ulemavu na magonjwa makubwa.

THE HERITAGE INSURANCE COMPANY TANZANIA LIMITED

Hawa wamejikita katika huduma ya bima inayohusu mambo ya mali, wizi, hatari zote katika biashara, sera katika usafirishaji wa mizigo, bima katika mahoteli, mizigo ya bandarini, masuala ya ajali za binafsi na za makund pamoja na bima nyingine nyingi.

Kwa ujumla, ni muhimu kutafakari ni bima gani ina umuhimu kwako kulingana na shughuli zako za kila siku au kutokana na maeneo yanayokuzunguka.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter