Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) kuzichukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuzifutia leseni za kufanyabiashara nchini kampuni za Bima kuwalipa wateja wao fidia za majanga kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya mali zilizokatiwa bima.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, ametoa maagizo hayo alipotembelea na kukagua mabanda ya maonesho katika maadhimisho ya pili ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza.
Alisema wahanga wamekuwa wakipata usumbufu wakati wa kudai fidia kwa kuwa hawalipwi kwa wakati na hata ukifika muda wanapolipwa fedha inakuwa imeshashuka thamani.
Amesema “malalamiko mengi yamekuja Wizarani kuhusu kampuni hizo za bima, naiagiza TIRA izichukulie hatua kampuni zote ambazo hazifuati sheria na taratibu”.
Ameiagiza pia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima kutoa suluhu kwa wakati na kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya nchi na kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinawajibika ipasavyo kwa matendo yao ili kuwawezesha wahusika kupata haki zao kwa wakati.
Aidha, aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukutana na benki na taasisi za fedha mbalimbali nchini kutafuta suluhu ya kupunguza riba za mikopo wanazowatoza wakopaji ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na mikopo ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Katika masuala ya masoko ya mitaji na dhamana, Chande aliiagiza Mamlaka ya Soko la Dhamana na Mitaji (CMSA) kuongeza wigo wa elimu kwa umma kuhusu dhamana hizo na namna mwananchi anavyoweza kunufaika kwa kuwa uelewa bado ni mdogo.