Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imetoa mikataba yenye thamani ya Sh. 1.44 bilioni kwa kampuni 23 kwa usambazaji huduma na uuzaji wa bidhaa nchini kwa mwaka 2017/2018. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya mamlaka hiyo, wanufaika wa tenda hizo ni kampuni binafsi na zisizo binafsi, lengo likiwa ni kuendeleza soko la bima nchini.
Taarifa hiyo imetaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni Winglink Travel Limited, PUMA Energy Limitedd, Fein One Investment Limited, BM Printers Limited pamoja na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Katika mkataba huo, kampuni ya PUMA imepata Sh. 329.82 milioni kwa ajili ya kusambaza mafuta kwa wafanyakazi wa TIRA. Aidha, GPSA imepata sh. 245 milioni kwa ajili ya usambazaji wa vyombo vya moto.
Mojawapo ya nia ya mamlaka hiyo ni kukuza uchumi wa nchi ambapo hadi sasa, soko la bima hapa nchini lina makampuni yanayotoa bima aina zote 25, kampuni nne zinatoa bima za maisha, na moja inatoa bima za jumla na za maisha ambapo kampuni hizi zina takribani madalali 99. Pamoja na hayo, kuna kampuni za nje zinazotoa huduma za bima 31 na madalali wa bima kutoka nje ni 41.