Baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa Tanzania imekataa kutoa ruhusa kwa ajili ya uchapishaji wa ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu mwenendo wa uchumi wa taifa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo vya kimataifa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema bungeni Dodoma kuwa hakuna zuio lolote na kwamba kinachoendelea hivi sasa ni mazungumzo ambayo ni sehemu ya utaratibu wa IMF.
Dk. Mpango ametoa ufafanuzi huo kufuatia maelezo ya Mbunge Frank Mwakajoka wa Tunduma (Chadema) aliyedai serikali imezuia shirika hilo kutoa ripoti wa uchumi wa taifa, wakati akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Kwa hiyo wasiwahishe mjadala, serikali bado inazungumza na IMF na hakuna sehemu ambayo imezuia, ni utaratibu wa IMF yenyewe”. Amesisitiza Waziri huyo.
Dk. Mpango amesema katika majadiliano hayo yanayofahamika kama Article 44 Consultants, wataalamu wa shirika hilo walikuwepo nchini mwaka jana mwishoni na baada ya hapo kutoa taarifa ambayo amedai kwa utaratibu inapaswa kurudi serikalini kwa ajili ya kutolewa maoni ambayo huzingatiwa kabla ya ripoti husika kuchapishwa.
“Na hiyo ripoti baada ya kuwa sisi tumepeleka maoni yetu, maoni hayajazingatiwa kwenye taarifa na nilipokuwa Washington juzi, nilizungumza na Mkurugenzi wa African Department na mpaka leo saa 9 bado tutaendeleza majadiliano kuhusu jambo hili. Na kwa utaratibu ni kwamba baada ya Executive Board ya IMF kuijadili taarifa hiyo, serikali inakuwa na siku 14 za kuipitia na kusema itolewe au isitolewe”. Ameeleza Waziri Mpango.
Amesisitiza kuwa mazungumzo baina ya serikali na shirika hilo yanaendelea na kwamba hakuna sehemu yoyote ambayo imezuiliwa.