Baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kukutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma, Majaliwa ametoa wito kwa bodi hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuagiza ifanye marekebisho ya maslahi kulingana na mazingira halisi ya mtumishi.
Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salaam katika makazi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amesema nia ya serikali ni kuhakikisha mishahara na maslahi ya watumishi wa umma nchini yanaboreshwa na kuitaka bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii.
Katika maelezo yake, Waziri Mkuu amesema serikali imeanzisha bodi hiyo ili kupata ushauri utakaotokana na tathmini sahihi ya nini serikali inapaswa kufanya ili kuboresha utendaji wa watumishi wa umma nchini.
“Tunataka muongozo mzuri wa kuwafanya watumishi wa umma wafanye kazi yao kwa waledi bila ya kuwa na vishawishi vya aina yoyote ikiwemo kuomba na kupokea rushwa”. Amesema Waziri Majaliwa.