Home FEDHA Mbinu za kuwa na mafanikio kifedha 2019

Mbinu za kuwa na mafanikio kifedha 2019

0 comment 130 views

Ukizungumzia mabadiliko, Mwezi Januari ni mwezi unaokuja na fursa mbalimbali za namna gani ya kuendesha maisha yako hususani upande wa kifedha. mwaka mpya ni muda wa kutafakari na kujipanga upya ili kubadili muelekeo wa maisha yako; hivyo badala ya kuwa na orodha ndefu ya mipango ambayo ni dhahiri kabisa huwezi kutimiza, njia bora zaidi kusonga mbele ni kujipanga kifedha kulingana na mazingira yako pamoja na hali halisi.

1. Kuwa na malengo ya kifedha

Malengo  na matarajio ya kifedha hutofautiana kulingana na mtu, lakini vyovyote vile, muda huu katika mwaka ni nafasi ya kipekee kujifunza kutokana na makosa ambayo huenda ulifanya, au kufikiria maeneo ambayo unaweza kujaribu kuboresha mwaka huu.

Chukua kalamu na andaa orodha ya vitu ambavyo hukuathiri kifedha na weka malengo ya miezi 12 inayofuata. Huenda unatumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye chakula na kutekeleza vitu vingine, andika vitu hivyo chini na tafuta suluhisho.

2. Andaa bajeti ya mwezi na mwaka

Bajeti binafsi ni tabia ngumu kujifunza lakini kuwa na uelewa wa hali yako ya kifedha ni hatua muhimu ya kufikia mafanikio ya kifedha. unapoanza bajeti yako jaribu mbinu ya 50/30/20- dhibiti mahitaji yako kwa 50%, unachotaka kwa 30% na weka akiba ya 20% ya kipato chako.

Orodhesha chote unachokipata na unachotumia na hifadhi taarifa hii. Watu wengi zaidi hutumia njia za digitali hivyo unaweza kutengeneza Excel na kujiwajibisha.

3. Weka rekodi ya matumizi yako

Kutunza  rekodi ni moja kati ya mambo muhimu ya kufanikisha bajeti yako. Hata matumizi madogo kabisa yataathiri bajeti yako, kutumia fedha na kutumia kiasi kidogo katika maeneo mbalimbali hupelekea kuongezeka kwa bajeti. Hivyo,jenga tabia ya kutunza risiti, zipitie na orodhesha matumizi yoyote ya ziada unayofanya ndani ya wiki.

4. Lipa madeni yako ya muda mfupi

Madeni, hasa ya muda mfupi, kama vile mikopo ya dharura yote yana nafasi pale ambapo ‘maisha hutokea’ lakini, hayapaswi kurundikana, hivyo weka kipaumbele katika kuyalipa mapema uwezavyo na kisha weka mipango ya kuweka akiba.

5. Kuwa na mfuko wa dharura

Mfuko wa dharura ni moja kati ya vipengele muhimu sana. Pale inapotokea umepata dharura ya kifedha  kama vile kuacha kazi, magonjwa au matumizi makubwa ya fedha ambayo hukuyategemea. Wataalamu wa masuala ya fedha hushauri kuwa na akiba ya angalau miezi mitatu ya gharama za kuendesha maisha – hata zaidi kama unaweza kufanya hivyo.

Usiruhusu matumizi usiyotegemea yaharibu mtazamo na mipangilio ya kifedha

6. Tengeneza malengo katika akiba

Kuliko kuwa na akiba nyingi bila mpangilio maalumu, gawanya akiba yako kwenye malengo au vitu maalumu ambayo unataka kutunza kama vile kusafiri, gharama kama vile ada ya shule pamoja na ukarabati wa nyumba.

Kufanya kazi kwa lengo la kutimiza ahadi fulani inarahisihia usimamizi. Weka malengo katika akiba yako na weka muda maalumu wa kufanikisha malengo hayo.

7. Epuka manunuzi makubwa

Kuwa na fedha za kumudu gharama kubwa haimaanishi kuwa unapaswa kufanya hivyo, kila matumizi ambayo yanapeleka kutumia kwa kipato chako cha mwezi huathiri bajeti yako na kupelekea athari ambazo zitakuwa za muda mrefu. Panga matumizi na yaongeze katika orodha yako ya malengo ya akiba ya muda mfupi.

8. Akiba ya malipo

Njia rahisi  ya kutimiza ahadi yako ya kuweka akiba ni kutengeneza  uhamisho wa moja kwa moja kuelekea kwenye akaunti yako ya akiba mara tu mshahara unapotoka. Kwa kufanya hivi, unaweka kipaumbele kwenye kuweka akiba na hushawishiki kutumia fedha hizo kwa ajili ya vitu vingine.

9. Kuwa na taarifa

Kuna mali kwenye kuwa na taarifa ili kufanikiwa kuwa na uhuru wa kifedha, ni muhimu kwa na taarifa kuhusu maamuzi ya kifedha unayoweza kufanya kubadilisha maisha yako. Mhudumu binafsi wa benki au Mtaalamu wa masuala ya kifedha ni chanzo kizuri cha kupata taarifa ambazo zitachochea mafanikio yako kifedha.

IMEANDIKWA NA DESIDERIA MWEGELO, MKUU WA KITENGO CHA MASOKO NA MAWASILIANO, STANBIC BANK.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter