Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imekanusha matangazo yaliyosambaa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameshiriki sherehe za uzinduzi wa mtandao wa tovuti inayotoa mikopo ndani ya dakika 45, www.boreshamaisha.ml . Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, wanaohusika na mtandao huo hawana uhusiano wowote na serikali ya Tanzania.
“Tovuti hii ya www.boreshamaisha.ml inaonyesha ni ya Malaysia wala sio ya Tanzania. Wanasema wanatoa mikopo hiyo kutoka mfuko wa VICOBA TANZANIA ambao umeanzishwa katika mfumo wa intaneti pekee (online). Wanadai wanatumia mawasiliano ya teknolojia kwa uchukuzi wa haraka kupitia tovuti kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa kila mtanzania popote alipo”. Imesoma taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo pia imeelezwa kuwa, waliofungua mtandao huo wametumia jina la Waziri Mkuu na hata kuweka picha yake akiwa bungeni Dodoma ambapo wamedai alipokea barua kutoka upinzani wakilalamika mikopo kutolewa kwa njia ya mitandao ni rushwa kwa ajili ya uchaguzi unaofuata (2020).
Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa wito kwa watanzania kujiepusha na mtandao huo ikisisitiza kuwa, sio halali na hauna nia njema kwa watumiaji.
“Kwa taarifa hii ya umma, tunapenda kuujulisha umma wa watanzania kwamba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hajashiriki uzinduzi wa tovuti hiyo, hana uhusiano wowote na watu hao na wala hana akaunti ya Facebook inayohamasisha watanzania wapate mkopo kwa dakika 45 kupitia njia ya mtandao”. Imeeleza taarifa hiyo.