Waziri wa maji Prof Makame Mbarawa, amesema Serikali imepokea mkopo wa Shilingi bilioni 210 kutoka Korea kupitia benki ya Exim na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kuboresha na kupanua mfumo wa maji taka Jijini Dar es Salaam. Waziri huyo amesema fedha hizo zitasaidia kuboresha mfumo huo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30 ambao unategemea kuelekezwa bahari ya hindi.
Pia ameongeza kuwa Serikali inafanya miradi kama hiyo Mkoa wa Arusha, Musoma na Sumbawanga huku mipango ikiendelea kuwekwa sawa kwa ajili ya Tanga.
Hadi sasa Mradi wa shilingi bilioni 78 wa maji taka unaendelea Jijini Arusha ambapo mfumo wa kisasa wa maji taka umejengwa na shirika linaloitwa Beijing Engineering Group.
Profesa huyo amesema kuwa mradi huo utakapotekelezwa jijini Dar es Salaam swala la maji taka kutuama hata mvua ikinyesha kidogo litapungua na kuisha .
Hata hivyo amewataka wananchi wa Tanga kutafuta pesa ili waweze kuunganisha mifumo ya kisasa ya maji taka na kuacha kuelekeza maji hayo machafu baharini kwa usalama wa afya zao na mazingira kwa ujumla.