Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga (TCAA) Hamza Johari amesema serikali ya Tanzania na Kampuni ya M/S Thales Air System ya nchini Ufaransa zimesaini mkataba wa ufungaji mitambo minne ya rada ambayo itagharimu Sh. 61.3 bilioni. Katika makubaliano hayo, Hamza amesema TCAA itagharamia asilimia 45 huku serikali ikigharamia asilimia 55 ya mradi huo.
Ameongeza kuwa mchakato wa kununua rada ulidhaminiwa mwaka jana na wafanyakazi kwa kutumia mapato ya ndani baada ya kushuhudia kuwa rada iliyopo sasa imepungua uwezo.
Hamza amedai kuwa mahitaji ya mitambo ya kisasa zaidi yametokana na ongezeko la ndege zinazotumia anga ya Tanzania, hivyo kuwepo kwa mitambo hii kutafanikisha urukaji wa ndege kwa kufuata viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Mradi huu unategemea kuchukua muda wa miezi 18ambapo rada zitafungwa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), KIA, Uwanja wa Ndege wa Songwe na Mwanza. Pia kuboresha miundombinu hii kutavutia ndege nyingi zaidi kuendesha shughuli zake katika anga la nchi yetu hivyo kuongezea nchi mapato kutokana na tozo za ndege zinazopita katika anga ya Tanzania.