Home FEDHA Waliofanikiwa hawana ‘time’ na mambo haya

Waliofanikiwa hawana ‘time’ na mambo haya

0 comment 92 views

Ili kupata mafanikio katika maisha ni muhimu kuwa tayari kufanya vitu kwa vitendo. Kuwa na wazo lenye thamani  ya mamilioni hakutakufanya uwe milionea kama hutalifanyia kazi. Watu waliofanikiwa walikuwa na wazo na wakalifanyia kazi, walikuwa wavumilivu na wakafikia malengo yao.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo watu waliofanikiwa hawafanyi:

Watu waliofanikiwa hawasubiri muda muafaka wa kuchukua hatua. Ni kawaida kwa watu kutoa sababu ya ‘muda sahihi’ jambo ambalo ni tofauti kwa waliofanikiwa kwani wao huamini kuchukua hatua bila kungoja hurahisisha kufikia malengo. Kwa kuendelea kusema muda bado unachelewesha mafanikio yako. Wanaoshindwa kufanikiwa hupenda kusubiri muda sahihi. Kwa bahati mbaya, hakuna wakati sahihi na njia pekee ya kuweza kufanikiwa ni kuchukua hatua na kuacha kusubiri.

Idhini kutoka kwa watu wengine. Moja ya sababu inayopelekea watu wasifanikiwe ni kujali watu wengine wanavyofikiria. Kitendo cha kusubiria idhini kutoka kwa familia au marafiki kinaathiri maisha na mafanikio yako kwa ujumla. Wakati mwingine sio lazima kufanya vitu ambavyo vitawafurahisha watu wengine. Unachotakiwa ni kuangalia ni je, kwa kufanya jambo hilo utanufaika?

Watu wenye mafanikio huwa na kawaida ya kuweka malengo yenye uhalisia. Unaweza kuwa na malengo makubwa lakini ni muhimu kutengeneza mikakati yenye uhalisia ili kufikia malengo yako kulingana na muda.

Sio vibaya kutamani mafanikio mengi, lakini ni muhimu kujua kuwa watu waliofanikiwa hawana malengo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu hata kuyafanyia kazi itakuwa ni changamoto. Angalia malengo yenye umuhimu zaidi na yanayotakiwa kufanyiwa kazi mapema. Unaweza kutengeneza orodha ya malengo ya muda mfupi na muda mrefu .

Watu waliofanikiwa hujua masuala gani yana umuhimu na yanahitaji kuzingatiwa zaidi. Huwezi kukuta mtu aliyefanikiwa analalamika kuwa ana majukumu mengi na mara nyingi, matokeo ya ufanisi wao wa kazi hueleza zaidi. Kanuni ya Pareto inaeleza kuwa matokeo ya jambo unalolifanya kwa 80% hutokana na juhudi zako kwa 20% hivyo ni muhimu kufikiria faida na hasara ya matendo yako ili kuepuka kutumia muda mwingi katika mambo yasiyo na umuhimu. Wakati watu wengi wanasema hawana muda kila wakati, watu waliofanikiwa hutenga muda kwa ajili ya mambo muhimu zaidi.

Siku zote kuchukua hatua ni rahisi lakini kupanga mipango madhubuti ni ngumu sana. Watu waliofanikiwa hujua kuwa ni muhimu kujipanga kabla ya kuchukua hatua. Mpango hupelekea kufanya utafiti na kujua mazuri na mabaya. Pia inakuwa rahisi kujua muda utakaochukua kufikia lengo lako na ujuzi gani unaotakiwa.

Watu waliofanikiwa hawana muda wa kuwanyooshea vidole watu wengine ikiwa makosa yamefanyika. Watu hawa huwajibika katika makosa yao na kuendelea na majukumu yao. Watu waliofanikiwa huwa tayari kupitia hali ngumu. Kwa kutengeneza mipango, kuomba msaada, kuachana na mambo ambayo hawawezi kubadilisha, na kutofanya maamuzi kwa hisia.

Watu wako wa karibu wanaweza kukurudisha nyuma hivyo watu waliofanikiwa huepuka watu wenye mawazo hasi na kutumia muda mwingi na watu wengine waliofanikiwa, wanaochochea maendeleo na mawazo chanya.

Huwezi kufanikiwa bila kujifunza, hivyo watu waliofanikiwa wanajua umuhimu wa elimu na huwekeza katika suala hili. Kusoma na kuhudhuria semina ni baadhi ya njia za kujifunza na kuongeza ujuzi.

Siku zote, wenye mafanikio hawakubali neno ‘hapana’. Usikubali kukatishwa tamaa na kuambiwa kuwa unachofikiria hakiwezekani. Endelea kujiamini, kujifunza na kuomba ushauri kutoka kwa wale wanaoamini katika mafanikio yako.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter