Kufuatia ujenzi wa vituo tisa vya biashara katika mipaka kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), biashara katika mipaka hiyo imeendelea kuimarika. Hotuba iliyosomwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda jijini Dodoma, imeeleza kuwa Tanzania ina njia 48 zinazoweza kupitisha bidhaa katika mipaka na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Congo, DRC, Zambia, Malawi na Msumbiji.
Pia inaelezwa kuwa vikundi 9 vya wafanyabiashara wanawake wadogo na wakati viliundwa na wanawake wa mpakani 292, hivyo kurasimisha biashara zao katika halmashauri nane nchini. Mbali na hayo, Waziri Kakunda ametaja vituo hivyo tisa vilivyopo mipakani kuwa ni: Holili/Taveta, Sirari/Isebania (Tanzania na Kenya), Namanga (Tanzania na Kenya), Kabanga/Kobero (Tanzania na Burundi), Rusumo (Tanzania na Rwanda), Mtukula (Tanzania na Uganda), Holoholo/Lungalunga (Tanzania na Kenya), Tunduma/Nakonde (Tanzania na Zambia), pamoja na Kasumulu/Songwe (Tanzania na Malawi).
“Hali ya biashara mipakani inaendelea vizuri na serikali imeendelea kutumia itifaki za umoja wa forodha na itifaki la soko la pamoja kurahisisha biashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya huku nchi za Zambia, Malawi na Msumbiji biashara inasimamiwa kupitia itifaki ya biashara ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika”. Amesema Waziri huyo.
Aidha ameeleza kuwa pamoja na kuchochea biashara, serikali ina mpango wa kuanzisha ujenzi wa masoko mipakani ili kukuza biashara na kuboresha maisha ya wakazi katika maeneo hayo.
Kakunda ametaja mikoa ambayo imeweka maeneo kwa ajili ya ujenzi wa masoko hayo kuwa ni Kagera (Mtukula, Murongo, Kabanga, Rusumo), Mara (Sirasi na Shirati), Mtwara (Kilambo na Mtambaswala), Ruvuma (Mbamba Bay na Mkenda), Kigoma (Kibirizi na Manyovu), Rukwa (Kirando, Kipuli, Kisanga, na Kasesya), Mbeya (Tunduma na Kasumulu), Tanga (Horohoro), Kilimanjaro (Tarakea), na Arusha (Namanga).