Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Denmark kuendeleza ushirikiano na Tanzania

Denmark kuendeleza ushirikiano na Tanzania

0 comment 100 views

Denmark imeahidi kuendeleza ushirikiano zaidi na Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na maendeleo ya wananchi kwa kutoa fedha na misaada ya kiufundi katika sekta ya mbalimbali ikiwemo afya.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissingspandet wakati akifanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamary Mwamba, katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.

“Denmark imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa miaka mingi kwa kusaidia utekelezaji wa bajeti ya serikali, kusaidia ujenzi wa mifumo ya udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali, kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na masuala ya afya kupitia ubia wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwenye Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI) ambapo ushirikiano huo umeleta matokeo chanya kwenye sekta hiyo,” amesema Mette.

Mette amepongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia maendeleo na kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya watu kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamary Mwamba ameishukuru Denmark kwa ushirikiano na mchango wao mkubwa katika kuendeleza sekta ya afya na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea pia kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma nzuri katika sekta ya afya na kutumia fursa za ushirikiano wa nchi hizo mbili kuwahudumia Watanzania.

Ushirikiano wa Tanzania na Denmark umetimiza zaidi ya miaka 60 na kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Denmark ikiwa ni baada ya mwaka mmoja tu tangu Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria ya Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 1962.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter