Akifuata nyayo za baba yake, Dk. Hussein Ali Mwinyi amegombea na kushinda nafasi ya urais wa Zanzibar.
Ushindi wake ulitangazwa siku ya pili baada ya kura kupigwa Oktoba 28 ambapo alitangazwa kushinda kwa asilimia 76 ya kura zote. Akisoma hotuba yake saa chache baada ya kutangazwa, raisi Mwinyi alisisitiza umoja na kutaka wananchi wa visiwani humo kuweka mbali tofauti zozote.
Alisema “ni muda sasa wa kutengeneza Zanzibar mpya. Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofauti zetu”.
Dk. Mwinyi amezaliwa Disemba 23, 1966, ni mtoto wa rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Baba yake alikuwa raisi wa awamu ya pili aliongoza kwa kipindi cha (1985-1995) baada ya alikuwa baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Tanzania bara ilifanya uchaguzi mkuu wa kuchagua Raisi, wabunge pamoja na madiwani Oktoba 28. Kwa utaratibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kura zilianza kupigwa Oktoba 27 kwa makundi maalum.
Wakati vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiripoti mapungufu na kasoro wakati wa uchaguzi, hakuna taarifa kutoka mamlaka husika juu ya ripoti hizo isipokuwa ile ya polisi ya kuwashikilia watu 70 ambao walihusishwa na uvunjifu wa amani.