Balozi wa Ireland Tanzania, Paul Sherlock amwaga sifa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuendeleza mtangamano na kusema Ireland itaendelea kushirikiana na nchi wanachama kukuza sekta ya biashara na kuleta maendeleo. Sherlock amesema hayo makao makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Biashara na Sekretariati ya EAC, Balozi Alhaji Rashid Kibowa pamoja na maofisa wa Idara hiyo.
Balozi huyo amesema uzoefu wa nchi ya Ireland katika Umoja wa Ulaya (EU) umedhihirisha kuwa kuna changamoto mbalimbali katika mtangamano na nchi wanapaswa zinapaswa kujadiliana ili kuzitatua.
Naye Balozi Kibowa amemueleza Balozi Sherlock kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata mafanikio makubwa kufuatia kutatua vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha biashara baina ya nchi. Vilevile, Balozi Kibowa amesema ili kukuza uchumi na kuboresha mazingira ya biashara, EAC imeanza mchakato wa kuwekeza kwenye maendeleo ya miundombinu kama bandari, barabara, nishati na reli.