Rais wa Tanzania, Samia suluhu Hassan amesema uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Kenya hauwezi kuvunjika akibainisha kuwa wapo watu wenye nia ovu wanaotamani kuona umevunjika.
Rais Samia amesema hayo Mei 5, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya.
“Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa. Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake, hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu.”
Ameahidi katika uongozi wake atahakikisha kuwa Kenya inabaki kuwa ndugu, jirani, mshirika wa mkakati na mbia kwa kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umefungwa katika mafundo matatu.
Rais Samia amesema “panapotokea ukame Tanzania njaa inabisha hodi Kenya, uzalishaji wa viwanda ukisimama Kenya bidhaa zinakosekana Tanzania hivyo hatuna budi kupatana na kuishi kwa neema na furaha.”