Kutokana na upungufu wa bidhaa ya viazi mbatata nchini Kenya, serikali ya Tanzania imeanza kupanga mikakati ya kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo ili wafanyabiashara wa viazi waweze kuuza nchini Kenya. Imeelezwa kuwa, kwa sasa mfuko mmoja wa viazi jijini Nairobi unauzwa Sh. 5,800 kutoka Sh. 3,500 ya awali.
Waziri wa Viwanda, Biashara, na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema hadi sasa, wamepata tenda mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki kwa mfano tenda ya kupeleka juisi nchini Uganda ambayo bado wanaishughulikia. Kakunda amesema kuwa wizara yake itaishughulikia ipasavyo fursa hiyo ya biashara.
“Wizara yangu iko makini kwa kila fursa wanayoona kufanyia kazi bila kuchelewa, hivyo kwa sasa tumeanza mikakati kukamata soko na tayari nimemuagiza Mkurugenzi wa TanTrade kuzungumza na wenzake wa Kenya ili tusikose fursa hiyo”. Amesema Kakunda.
Hata hivyo,seikali ya Kenya inasema inafanya jitihada zote kuhakikisha bidhaa hiyo inakuwepo kwa uhakika kwa wakulima kutumia mbegu zinazofaa wakati wa uzalishaji.