Home Elimu ELIMU YA UJASILIAMALI YAOMBWA KUANZIA CHINI

ELIMU YA UJASILIAMALI YAOMBWA KUANZIA CHINI

0 comment 83 views

Tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi katika jamii zetu za kiafrika. Kuna zile nchi ambazo uchumi wao unakua kwa kasi huku nyingine huku nchi nyingine ukuaji ukiwa wa taratibu.

Shughuli za ujasiliamali katika nchi za Afrika Mashariki kama zilivyo nchi nyingine duniani zinafanyika lakini si kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na jamii nyingine kama Ulaya. Hali hii inatokana na mazingira halisi ya nchi hizi ikiwamo ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya ujasiliamali, Ukosefu wa mitaji kuendeshea biashara sambamba na kasumba za watu kuhusiana na ujasiliamali.

Nchi za Afrika Mashariki kama zilivyo nchi nyingine duniani hata zilizoendelea kiuchumi, bado  zinakabiliwa na suala la uhaba wa ajira, tatizo ambalo sasa limekuwa sugu. Kumekuwepo na idadi kubwa ya vijana mtaani ambao wanamaliza masomo yao lakini kutokana na vitu hivi vitatu vilivyoainishwa hapo juu, wamebaki kuishia vijiweni na stendi za mabasi huku wengine ukipishana nao na bahasha zao za khaki wakihangaika huku na huko kutafuta ajira.

Ni dhahiri kuwa serikali zinatambua kuwa katika kizazi hiki kumekuwepo na uhaba wa ajira duniani hivyo zimekuwa zikichukua hatua stahiki za kuondoa mrundikano wa watu wasio na kazi  mtaani kwa kutoa elimu inayowaandaa watoto tangu wakiwa wadogo kujifunza ujasiliamali na namna ya kujitegemea pindi wanapomaliza masomo yao.

ADVERTISEMENT

Robert T. Kiyosaki ni mjasiliamali na mwandishi wa vitabu mbalimbali. Katika kitabu chake cha Rich Dad Poor Dad amehimiza mtoto kufundishwa kuhusu ujasiliamali kuanzia umri wa miaka 9. Wanawafundisha watoto namna ya kujishughulisha na ujasiliamali kama njia ya kuwaandaa na maisha ya baadae, tofauti na elimu ya nchi nyingi za Afrika Mashariki inayomwandaa kijana kuajiriwa.

Kwanini elimu ya ujasiliamali itolewe kuanzia shule za msingi?

  1. Kupunguza utegemezi.

Vijana wengi katika nchi za Afrika Mashariki wamegeuka kuwa tegemezi kwa wazazi wao baada ya kumaliza masomo yaona kukosa ajira. Hii inatokana na kutokuwepo kwa mtaala bora unaowaandaa kwenda kujitegemea baada ya kumaliza masomo yao. Hivyo kama elimu itatolewa kwao tangu wakiwa wadogo itawafanya wajijenge katika kujiamini na kujua kuwa huko mbeleni watahitaji kujitegemea.

  1. Kuandaa taifa shupavu na vijana wachapakazi.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2005 kwa kumbukumbu za haraka kuna vitabu vilikuwa vikitolewa vilivyoandikwa Sayansi Kimu. Vitabu hivi vilikuwa vikitoa elimu mbalimbali inayohusiana na kilimo pamoja na ufugaji ikiwa ni pamoja na namna ya kuandaa shamba vizuri, kupanda mimea au kuotesha shambani na namna gani kilimo kinaweza kukufanya ukafanikiwa kimaisha. Hivi vitabu bado vina umuhimu kwa jamii ya sasa. Endapo mtaala wa elimu ya ujasiliamali utakuwepo shuleni na hii elimu ya kilimo, biashara na ufugaji ikapewa mkazo kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni ni dhahiri kutakuwepo na kizazi cha wachapakazi na watu shupavu katika jamii watakaoweza kujitegemea na kuendesha maisha yao wenyewe.

  1. Kupunguza tatizo la ajira mtaani.

Endapo elimu ya ujasiliamali kwa vitendo itatolewa kuanzia shule ya Msingi hadi vyuoni ni dhahiri kuwa watu hawa watakuwa wamekomaa kiasi cha kutosha kwa ajili ya kujitegemea. Ni ukweli kuwa elimu ya ujasiliamali imekuwa ikitolewa katika kozi mbalimbali katika ngazi ya chuo lakini si elimu ya vitendo bali imejikita katika nadharia tu. Jamii haiwezi kusonga mbele endapo elimu ya ujasiliamali haitapewa kipaumbele.

Nini kifanyike ili kujenga kizazi bora na chenye kujitegemea?

Kuondoa dhana mbovu ya ujasiliamali. Watu wengi mpaka sasa wanaamini kuwa mamalishe ndio mjasiliamali ila mtu kama Mo Dewji ni mfanyabiashara. Ujasiliamali ni neno lenye fasili pana tofauti na mtazamo huo. Ujasilimali ni kitendo cha kufanya biashara huku ukichukua tahadhari kwa lengo la kupata faida zaidi. Hivyo kama taifa, inatakiwa:

  1. Kuwaandaa vijana kujiamini na kutokata tamaa. Vijana lazima waandaliwe katika kuchukua tahadhari katika biashara, wakipata hasara wafanye nini ili kurudi pale wanapostahili kuwepo, namna gani waweze kuvuka malengo waliyojiwekea katika shughuli zao za ujasiliamali
  2. Kuandaa warsha, makongamano na semina mbalimbali zinazohusiana na ujasiliamali sehemu mbailimbali za nchi. Serikali na wadau binafsi wana wajibu wa kuandaa warsha, makongamano na semina mbalimbali zinazohusiana naujasiliamali ili kuwandaa vijana na kuwaonyesha fursa mbalimbali za ujasiliamali katika mazingira yanayowazunguka.
  3. Kuwapatia mitaji ikiwa ni sambamba na utoaji wa mikopo. Hii itawasaidia kuwa na sehemu ya kuanzia maana kwa asilimia kubwa ujasiliamali unahitaji mtaji. Hivyo endapo serikali na taasisi binafsi zitasaidia katika kutoa mikopo itawapa vijana hawa mwanya wa kuzifanyia kazi fursa hizo.
  4. Kuhamasisha vijana kujiunga na vikundi vya uchangiaji fedha mfano VICOBA. Vikundi hivivina umuhimu katika jamii kwa sababu licha ya kwamba vinawasaidia vijana kukuza mitaji yao lakini pia wengine wamekuwa wakipata uzoefu wa kile wanachokifanya wenzao baada ya kuchangishiwa hiyo fedha.

Kwa ujumla suala la ujasiliamali katika kizazi hiki halipingiki na halijachelewa bali ni suala la serikali, wadau binafsi na taasisi mbalimbali kuona umuhimu wa kuhimiza watoto kuandaliwa mapema namna ya kujitegemea na kujihusisha katika ujasilimali lakinipia kwa vijana nao pia bado wana  nafasi kwa ajili ya kuchukua hatua kadhaa ya kujikwamua  pale walipo na kuziangalia fursa zilizo mbele yao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter