Viazi vitamu ni moja kati ya mazao makuu ya mizizi. Kutokana na uwezo wake wa kuvumilia ukame, zao hili ni moja kati ya mazao ya kinga ya njaa. Hapa nchini, zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma. Kuna aina mbalimbali za viazi vitamu zikiwemo Ukerewe, Kakamega, Karoti C, Mavuno, Pananzala na Polista.
Zao hili hustawi maeneo mengi hapa nchini na hukubali vizuri zaidi katika maeneo ya tambarare yenye udongo tifutifu ambao unaruhusu maji kupenya kirahisi. Udongo mfinyazi na wenye kokoto nyingi haufai kwa ajili ya kilimo hiki kwani huzuia mizizi kupenya na kupanuka.
Kabla ya kuanza rasmi kilimo cha viazi vitamu, mkulima anapaswa kuhakikisha shamba linatayarishwa vizuri kwa kufyeka vichaka na kung’oa visiki. Vilevile, majani yanatakiwa kufunikwa wakati wa kutengeneza matuta ili kuiongezea udongo rutuba.
Wataalamu wanashauri kupanda viazi kwa kutumia mashina yenye urefu wa sentimita 30 kwa matokeo mazuri zaidi. Inashauriwa kutumia sehemu ya juu ya shina kuongeza mavuno. Mashina yanatakiwa kupandwa katika umbali wa sentimita 25 hadi 30 kutoka mmea hadi mmea na sentimita 60 hadi 75 kutoka tuta hadi tuta. Viazi pia vinaweza kupandwa kwa kutumia viazi vyenye afya na vyenye uzito wa gramu 20 mpaka 30.
Mkulima anatakiwa kupalilia shamba miezi miwili ya mwanzo ili kuwezesha mmea kutambaa vizuri. Baada ya muda huo, viazi huweza kufunika ardhi na hivyo huzuia uotaji wa magugu. Wadudu kama vile kipepeo, mbawa kavu, fukusi na minyoo fundo ni baadhi ya changamoto za aina hii ya kilimo. Viazi vitamu pia hushambuliwa na magonjwa mbalimbali yatokanayo na virusi. Magonjwa haya pamoja na uwepo wa wadudu yanaweza kudhibitiwa kwa usafi, kubadilisha mazao pamoja na kuzingatia udhibiti sango.
Kilimo cha viazi vitamu ni kwamba huchukua muda mfupi tu kukomaa, hivyo mkulima anaweza kupata faida mapema. Mara nyingi viazi huwa tayari kuvunwa kuanzia miezi mitatu hadi minne tangu kupandwa kulingana na hali ya hewa. Viazi huvunwa kidogo kidogo kwa kutumia mikono, vijiti, jembe au rato. Mkulima anatakiwa kuhakikisha viazi haviachwi ardhini kwa muda mrefu bila kuvunwa kwani vitakomaa kupita kiasi na kuharibu ubora wake. Uvunaji unapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha viazi havikatwi wala kuchubuliwa wakati wa zoezi hili.
.