Watumiaji wa iPhone 5 wamepokea ujumbe wa pop-up katika siku za hivi karibuni kutoka katika kampuni ya Apple, ambapo kampuni hiyo inawahimiza watumiaji wa simu hizo kusasisha(update) toleo la iOS kwenda katika sasisho la kisasa ambalo ni iOS 10.3.4. Watumiaji wa simu hiyo wametakiwa kufanya mabadiliko hayo hadi tarehe 3 mwezi ujao, na ikiwa mtumiaji hatofanya mabadiliko basi hatoweza kutumia mtandao wa intaneti katika simu hiyo ikiwa ni pamoja na programu zinazotumia intaneti katika simu hiyo kwamfano programu ya App Store, tovuti,GPS huduma ya iCloud nk.
Mchakato mzima wa kusasisha kwenda katika toleo jipya katika aina hiyo ya simu unaweza kufanyika bila waya (wireless-kwamfano Wi-Fi) au kwa kutumia kompyuta kabla ya tarehe tatu, baada ya hapo watumiaji watatakiwa kuunganisha simu hiyo katika kifaa cha Mac au PC kwani sasisho zisizotumia waya (wireless) hazitaweza kufanyika tena.
Iphone 5 inaweza kusasishwa kwa urahisi ambapo mtumiaji atatakiwa kufuata maelekezo haya: na kwenda katika programu ya ‘Settings’ na kubonyeza ‘General’ kisha ‘Software update’ baada ya hapo mchakato wa kusasisha utaanza kufanyika. Ikiwa bado simu inahitaji kusasishwa basi ujumbe utakuja tena ukieleza kuwa inahitajika kupakua sasisho jipya.
Kwa sasa mfumo wa uendeshaji wa Apple umefika iOS 13. Lakini iOS 10.3.4 ndio mfumo wa kisasa ambao unaweza kufanya kazi katika simu ya iPhone 5.Aidha, imeelezwa kuwa simu janja hiyo ilizinduliwa mwaka 2012, na kuuza takribani simu milioni 70.