Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (MB) ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kujipanga kuhudumia shehena ya mzigo wa Malawi kutoka asilimia 20 hadi 100 kuanzia sasa.
Waziri Kamwelwe ametoa agizo hilo siku ya Ijumaa Machi 29, 2019 wakati wa kikao cha pamoja baina yake na Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi wa Malawi, Mhe. Jappie Mhango (MB) kilichofanyika jijini Dar es Salaam. “Hivi karibuni kumetokea mvua kubwa ambazo zimesababisha uharibifu mkubwa kwenye Bandari ya Beira nchini Msumbiji pamoja na nchi ya Malawi ambayo awali ilikuwa ikiitumia Bandari hiyo kupitishia mzigo wa Malawi, kutokana na uharibifu huo sasa Malawi wataitumia Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 100 badala ya asilimia 20 ya awali,” amefafanua Waziri Kamwelwe.
Waziri amesema kwamba Bandari ya Beira kwa sasa imeoshwa kabisa na mafuriko yaliyotokea na jambo hilo sasa linaifanya Malawi kuanza kutumia Bandari za Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia mia moja.
Pamoja na hilo Waziri Kamwelwe amesema maamuzi ya kutumia Bandari za Tanzania pia yametokana na mazungumzo ambayo ameyafanya na Waziri mwenzake wa Malawi yaliyolenga kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya nchi za Tanzania na Malawi.
Ameongeza kuwa mkutano wake na Waziri mwenzake pia umelenga kuona mahusiano baina ya nchi hizi mbili yalianza wapi na wapi wanaweza kuboresha na wamegundua kuwa tayari kulikuwa na mkataba wa mahusiano kati ya Tanzania na Malawi ambao ulisainiwa na Mawaziri wa Uchukuzi mwaka 1987. “Bahati nzuri tumeupata na tumeupitia mkataba huo wa mahusiano ambao kimsingi ndio uliifanya Serikali ya Malawi ikajenga Bandari kavu ambazo leo zinazojulikana kama Malawi Cargo hapa Dar es Salaam na Mbeya,” amefafanua Waziri.
Amesema kuwa ili kuendelea na utekelezaji wa mkataba huo wamekubaliana kuunda timu ambayo itapitia mkataba huo ambao kimsingi haujawahi kufanyiwa marekebisho ili uweze kukidhi matakwa ya sasa ya kisheria, taratibu na kanuni kwa lengo la kuingiza mabadiliko yatakayokidhi mahitaji ya sasa ya kijamii na kibiashara.
Chanzo:Bandari(Tanzaniaportshq)