Home Uncategorized Mashua ya plastiki yatua Zanzibar, UN yapongeza SMZ kwa kukabili taka za plastiki

Mashua ya plastiki yatua Zanzibar, UN yapongeza SMZ kwa kukabili taka za plastiki

0 comment 112 views

MRATIBU wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kusimama kidete kupambana na taka za plastiki.

Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja wa Mataifa wakati wa hafla ya mapokezi ya mashua iliyotengenezwa kwa plastiki iluyotia nanga kwenye fukwe za Forodhani yenye kupeleka ujumbe wa kupambana na taka za plastiki baharini na fukwe visiwani Zanzibar.

Aidha alisema kutokana na dhamira ya dhati  ya kukabiliana na taka za plastiki taifa hilo linatekeleza mkakati wa kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa taifa pamoja na kufikia malengo ya maendeleo endelevu hasa lengo namba kumi na nne la kulinda uhai chini ya maji na lengo namba kumi na tano la kulinda uhai juu ya ardhi.

Mratibu huyo alisema hayo kwenye mapokezi ya mashua iliyotengenezwa kwa plastiki mjini hapa yenye kupeleka ujumbe wa kupambana na taka za plastiki baharini.

Katika hafla hiyo ambayo viongozi wengi wakiwemo wa serikali walihutubia, Alvaro aliipongeza Tanzania kwa kutenga maeneo ya hifadhi kwa ajili ya manufaa ya wananchi na dunia kwa ujumla na kutia saini mikataba mbalimbali ya hifadhi ikiwamo viumbe wanaotoweka.

Mashua hiyo iliyotengenezwa kwa kutumia mabaki ya plastiki yaliyokusanywa kutoka katika fukwe za Kenya, imeingia nchini juzi ikitokea kwenye mji wa Lamu.

Mashua iliyotengenezwa kwa taka za plastiki ikiwa imetia nanga kwenye fukwe za Forodhani visiwani Zanzibar iliyofanya safari kutokea LAMU-ZANZIBAR huku njiani ikiendelea na kampeni ya kuhamasisha kupambana na taka za plastiki baharini na fukwe kupitia Mashua hiyo.

Mashua hii iliyosafiri umbali wa kilometa zaidi ya 500 imesimama katika visiwa kadhaa ili kueneza ujumbe kuhusu madhara yanayotokana na matumizi ya plastiki katika bahari.

Hassan Shafi mmoja wa waliounda mashua hiyo, anasema kilichosababisha ubunifu huu ni uwapo wa takataka nyingi za plastiki ambazo zinapatikana baharini na katika fukwe zinazotishia mazingira ya bahari na viumbe hai.

Alvaro katika mazungumzo yake alisema kutokana na kuzagaa kwa takataka upokeaji wa kampeni ya kusafisha bahari dhidi ya taka za plastiki unaonesha ni kwa namna gani Tanzania ipo tayari kuhifadhi mazingira kwa malengo hayo mawili.

Alisema tatizo la uchafuzi wa bahari limekuwa ni la kidunia na changamoto zake zinaangukia kwa wanaozunguka bahari.

Wakazi wa visiwani Zanzibar wakiwemo wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na watalii wakishiriki zoezi la kusafisha pembezoni mwa fukwe za Serena Hoteli kwa kuokota taka za plastiki ikiwa ni kampeni ya kuhamasisha kupambana na taka za plastiki baharini na fukwe visiwani Zanzibar.

Alisema dunia inatakiwa kuchukua hatua kama Zanzibar za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na pia mirija ya kunywea soda, chupa za plastiki na kuendesha kampeni vyombo vya baharini kuacha kutupa uchafu wa plastiki baharini.

Pamoja na juhudi hizo ametaka kuongezwa kwa jitihada zaidi hasa katika kuelimisha jamii kuchukua jukumu la kutunza mazingira na kupambana na uchafuzi wa plastiki.

Alisema juhudi lazima zifanyike ili kuhakikisha kwamba tishio la kupoteza viumbe wanaoishi baharini katika miaka 30 ijayo linafutwa.

“Utafiti uliofanywa na UNEP unaonesha kwamba dunia itapoteza samaki na viumbe wengine wa baharini miaka 30 ijayo kama kasi ya uchafuzi wa mazingira kwa plastiki utaendelea kama ulivyo sasa” alisema.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Kimataifa la Mazingira (UN Environment Assembly-UNEA), Siim Valmar Kiisler ambaye alifika nchini kwa ajili ya hafla hiyo, akizungumza na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Mohamed Abood ofisini kwake Vuga, alisema wananchi wengi wanaozungukwa na ukanda wa bahari wapo hatarini kukabiliwa na magonjwa mbalimbali kutokana na ulaji wao wa  samaki ambao nao wengi huguguna taka za plastiki kama chakula chao cha kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Rais wa Baraza Kuu la Kimataifa la Mazingira (UN Environment Assembly-UNEA), Siim Valmar Kiisler aliyefika ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo. Kushoto ni Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez aliyeambatana na ugeni huo visiwani Zanzibar.

Alisema watu wengi wamekuwa wakifurahia ulaji wa samaki bila ya kufahamu chakula anachokula samaki kuwa kinaweza kuwa na sumu isiyoweza kuonekana wala kuathiri kwa haraka.

Alieleza katika kujiepusha na mazingira hayo hatarishi jamii haina budi kutunza na kuenzi mazingira ya bahari ikiwemo kuacha tabia ya kutupa taka zote za plastiki katika maeneo ya bahari.

Rais wa Baraza Kuu la Kimataifa la Mazingira (UN Environment Assembly-UNEA), Siim Valmar Kiisler akishiriki zoezi la kusafisha pembezoni mwa fukwe za Serena Hoteli kwa kuokota taka za plastiki ikiwa ni kampeni ya kuhamasisha kupambana na taka za plastiki baharini na fukwe visiwani Zanzibar.

‘’Kuna watu ndani ya jamii yetu hususani wanaoishi kwenye ukanda huu wa bahari wanashindwa kujua kuwa taka zitokanazo na plastiki huweza kudumu hadi kwa miaka 500 baharini bila kuharibika’’aliongezea.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Waziri wa Nchi ofisi ya Makamo wa pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alisema kuna changamoto mbali mbali za utunzaji na uhifadhi wa mazingira visiwani hapa.

Mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mohammed Aboud Mohammed akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya mashua iliyotengenezwa kwa plastiki iluyotia nanga kwenye fukwe za Forodhani yenye kupeleka ujumbe wa kupambana na taka za plastiki baharini na fukwe visiwani Zanzibar.

Alisema jamii bado ina mwamko mdogo wa kutunza mazingira jambo ambalo amekiri kuwa ni changamoto ambayo inahitaji kusimamiwa ipasavyo.

Hata hivyo alisema anaamini ujio wa mashua hiyo iliyotengezwa kwa taka za plastiki utaleta ujumbe tosha kwa wananchi wa Zanzibar na maeneo mengine kuhifadhi mazingira yao yanayowazunguka.

Tags:

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter