Home Uncategorized Sababu 3 za kuwa na kitambulisho cha taifa

Sababu 3 za kuwa na kitambulisho cha taifa

0 comment 267 views

Katika kila taifa kuna umuhimu kwa wananchi kuwa na vitambulisho vya taifa(NIN) ili kuweza kujua wananchi wanaoishi katika taifa husika kihalali ikiwa ni pamoja na kutambua shughuli wanazojihusisha nazo. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekuwa ikihamasisha watanzania kupata vitambulisho hivyo ili kuchochea usalama na amani kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika taifa.

Kupitia vitambulisho hivyo mambo mengi yatarahisisha ikiwa ni pamoja na usajili wa namba za simu na mengineyo. Lakini je, katika upande wa biashara na uchumi wa nchi kuna faida gani za kuwa na kitambulisho cha taifa? Zifuatazo ni sababu 3 za kila mfanyabiashara na mtanzania kuwa na kitambulisho hicho:

Kurahisisha umiliki katika biashara

NIDA inawahamasisha watanzania kuwa na kitambulisho cha taifa ili kurahisisha suala zima la umiliki katika biashara ikiwa ni pamoja na suala zima la usajili wa biashara nchini. Ambapo kila mfanya biashara mpya au ambaye tayari anafanya biashara anatakiwa kuwa na kitambulisho hicho ili kuirahishia serikali kujua idadi ya wafanyabiashara nchini na kujua wafanyabiashara wanaofanya biashara halali nchini. Hivyo kama mfanyabiashara makini unatakiwa kuwa na kitambulisho hicho ili kuepukana na changamoto ya usajili wa kampuni au biashara (BRELA) ambako watahitaji kitambulisho hicho ili kufanya mchakato mzima.

Kurahisisha ukusanyaji wa mapato

Baada ya serikali kupata idadi kamili ya wafanyabiashara nchini kupitia vitambulisho vya taifa ambavyo hutumika pia katika usajili wa biashara itakuwa rahisi kwa mamlaka ya mapato nchini (TRA) kukusanya mapato nchini ili kuweza kuendeleza uchumi wa nchi kuelekea katika uchumi wa kati.

Ni rahisi kujua watu wanaonufaika na mifuko ya kijamii

Kupitia vitambulisho vya kitaifa itakuwa rahisi kufahamu watu wanaonufaika na mifuko ya kijamii kwa mfano malipo ya pensheni, haki za matibabu, masuala ya kimasomo pamoja na stahiki zote ambazo watanzania wanastahili kuzipata. Kwasababu kupitia kitambulisho mtanzania yeyote atatambulika kirahisi kuwa yeye ni nani, yuko wapi, na anafanya nini.

Aidha, kutokana na changamoto mbalimbali za kupata namba ya utambulisho wa Taifa (NIN), NIDA imewarahishia watanzania kufanya mchakato huo kwa kuweka huduma hiyo katika mtandao, licha ya taasisi hiyo kupeleka namba za watu ambao wameshaomba vitambulisho hivyo katika ofisi za kila kata nchini.

Kupitia tovuti yao ya www.nida.go.tz mtu anaweza kujisajili bila ya kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter