Home Uncategorized Uzalishaji miche ya mkonge kwa chupa kufikia milioni 10

Uzalishaji miche ya mkonge kwa chupa kufikia milioni 10

0 comment 186 views

Serikali imepanga kuzalisha miche milioni kumi kwa njia ya teknolojia ya chupa (Tissue Culture) kupitia maabara ya kisasa inayojengwa katika Kituo cha Utafiti TARI Mlingano, Wilaya ya Muheza, Tanga.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amebainisha hayo alipotembelea kituo cha TARI Mlingano na kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo.

“Mahitaji ya miche ya mkonge ni takribani milioni 11 kwa mwaka, wakati uwezo wetu kwa sasa kupitia TARI ni wastani wa miche milioni 5 tu kupitia njia zote yaani ya vikonyo na chupa. Wakulima wengi waliokuwa wameacha kulima mkonge wamehamasika kurudi kupanda zao hili la kimakati.

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija. Na ndiyo maana mnaweza kuona kipindi cha miaka 2 hii, bajeti ya utafiti imeongezeka kutoka wastani wa bilioni 11.7 hadi bilioni 43 ili kuwezesha kufanya utafiti wa mbegu bora zitakazoleta manufaa kwa wakulima,” amesema Mavunde.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuwajengea uwezo watafiti ili waweze kufanya tafiti ambazo zitakuwa na tija na zinazoendana na wakati uliopo sasa ambazo zitakuwa na manufaa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

“Msimu uliopita uzalishaji wa mkonge ulifikia tani 48,513. Kwa msimu huu, kwa kipindi cha Januari hadi Julai 2023 takribani tani 34,000 zimezalishwa, ambazo zimetuletea fedha za kigeni Dola za Kimarekani milioni 41 na fedha za ndani Shilingi bilioni 23, mtaweza kuona ambavyo mkonge unaendelea kufanya vizuri,” amesema Mavunde.

Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Mlingano, Dkt. Catherine Senkoro ameeleza kuwa hapo nyuma walikuwa wakizalisha miche 500,000 pekee ambapo baada ya kuboresha kwa sasa wanazalisha miche milioni 5 ambayo bado haikidhi mahitaji.

Amesema uwepo wa maabara hiyo ni mkombozi kwa wakulima ambao wamekuwa wakihitaji sana miche bora ya mkonge.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter