Baada ya mgodi wa dhahabu wa North Mara (Acacia) kushindwa kujenga bwawa jipya kwa ajili ya kuhifadhi maji yenye sumu na kuyazuia kutiririka kwenye makazi ya watu, serikali imeutoza mgodi huo faini ya Sh. 5.6 bilioni. Waziri wa Madini, Doto Biteko pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) January Makamba wamechukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mgodi huo na kushuhudia ukiukwaji wa Sheria na uchafuzi wa mazingira ambao umepelekea wananchi kupata madhara na wengine kupoteza maisha kutokana na kutumia maji yenye sumu.
“Tangu wananchi waanze kulalamikia maji haya kuwa ni machafu na yana sumu, leo ni miaka 10 sasa tangu mwaka 2008 hadi mwaka huu serikali ilipothibitisha kuwa kweli yana sumu. Baada ya vipimo kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali na kubainika yana sumu, leo tumefanya ziara na tumethibitisha kuwepo kwa maji haya yenye sumu”. Amesema Makamba.
Mbali ya kutozwa faini, mgodi huo pia umepewa muda wa wiki tatu kukamilisha uchimbaji wa bwawa jipya ya kuhifadhi maji yenye sumu na endapo watashindwa kutekeleza agizo hilo, serikali itasimamisha leseni yake ya uchimbaji.
Kwa upande wake, Waziri Biteko amesema serikali itapitia upya tathmini ya fidia ya malipo ya wananchi na kuagiza migodi yote kuzingatia Sheria za uchimbaji.